Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtaalamu atoboa siri ya mavuno kidogo kahawa

806a4101b92b1022cc34f7c4c099d41c Mtaalamu atoboa siri ya mavuno kidogo kahawa

Sun, 19 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKOA wa Mkoa wa Kagera unapoteza tani 31,000 za kahawa safi kila mwaka. Hali hiyo inatokana na wakulima wengi kuendelea kushikilia mibuni ya zamani, ambayo imepandwa kwa zaidi ya miaka 50 hadi 70.

Hayo yalisemwa jana na Mtafiti Mwandamizi Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI) mkoani Kagera, Dk Nyambisi Ng’homa.

Alisema utafiti uliofanyika unaonesha kuwa mkoa wa Kagera unaweza kupata zaidi ya tani 60,000 za kahawa safi, lakini umesalia kupata tani 29,000 tu kutokana na kutopandwa mibuni mipya.

Alisema mibuni huanza kupunguza uwezo wa kuzalisha kahawa nyingi, inapofikisha miaka 10 tangu kupandwa. Kwa sasa kila mbuni mmoja mkoani Kagera, unatoa wastani wa nusu kilo ya kahawa safi, badala ya kilo moja na nusu.

Dk Nyambisi alisema wakati serikali inahamasisha kilimo chenye tija, ni vema ihamasishe watu kupanda mibuni mipya au kusaidia mibuni ya zamani kuirudisha katika ujana, hali itakayosaidia kupata mavuno yanayotakiwa.

Alisema changamoto ya kuvuna mavuno kidogo, itatatuliwa na shirika lisilo la kiserikali la Cafe Afrika kwa kushirikiana na wadau wa kahawa mkoani Kagera. Shirika hilo linaendesha mradi wa miaka mitano wa kilimo cha kahawa.

Meneja Mradi wa shirika hilo, Daniel Mwakalinga alisema kuwa kupitia mradi huo wameanzisha vitalu vipya vya miche ya kahawa na kuweka miundombinu ya kupandia miche hiyo.

Miundombinu hiyo inawezesha pia miche hiyo kukabiliana na magonjwa. Pia, shirika hilo limetoa vifaa kwa wakulima na maofisa ugani wapatao 450 wanaotoa elimu shambani, kuhamasisha kilimo bora na kusaidia vijana kuwekeza katika mashamba ili kuongeza uzalishaji. Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheruka aligawa vifaa kwa wakulima vijana, waliopata mafunzo ya ugani yatayowasaidia wakulima wengine kufufua mashamba yao.

Aliwaagiza maofisa kilimo kufanya ziara mashambani kila mwezi, ili mafunzo yaliyotolewa yawasaidie wakulima. Alisema kuwa wilaya ya Karagwe imetenga ardhi kwa ajili ya kilimo cha kahawa.

Kuna mashamba darasa kwa ajili ya vijana, ambao wanapatiwa hekari moja kila mmoja kupanda mibuni mipya na kuongeza uzalishaji. 

Chanzo: habarileo.co.tz