Dar es Salaam. Baadhi ya taasisi za Serikali ya Tanzania zimetakiwa kutotumia nguvu kurasimisha biashara ili kuwafanya wafanyabiashara kutokimbia sekta rasmi kwenda sekta isiyo rasmi.
Rai hiyo imetolewa leo Alhamisi Julai 4, 2019 na Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi wakati akifanya uchambuzi wa bajeti ya Serikali ya Tanzania mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni kwa wakurugenzi wa asasi za kiraia.
Profesa Ngowi amesema ukusanyaji wa mapato unahitaji elimu na kuwajengea wananchi utamaduni wa kulipa kodi wenyewe bila kusukumwa na mamlaka za Serikali
"Baadhi ya wafanyabiashara walifunga biashara pale Kariakoo kwa sababu ya kusumbuliwa, sasa wameamua kuwapa vijana bidhaa zao watembeze mitaani. Serikali inakosa mapato yake," amesema
Amesema bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 inavutia wawekezaji kwa kupunguza kodi, “Ila haitoshi inatakiwa pia kuwashikilia wasiondoke kwa kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji.”