Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msimu ujao wa korosho utakuwa hivi

48441 Pic+korosho

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu wengi wanajiuliza maswali lakini huenda hawapati majibu kuhusu namna msimu ujao wa korosho utakavyokuwa baada ya ule wa mwaka huu kuwa na changamoto ya bei jambo lililoilazimu Serikali kuingilia kati kuinunua.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema msimu ujao hautakuwa na tofauti kubwa na wa sasa, lakini utakuwa rafiki zaidi kwa wawekezaji wa ndani hususan wanaoongeza thamani.

Alisema utaratibu ndio utakaotumiwa pengine na nchi zote za Afrika.

“Tunataka mazao yetu yaongezewe thamani ndani ya nchi ili tutengeneze ajira kwa watu wetu na kuongeza pato la Taifa. Wenye viwanda vya kubangua korosho wasiwe na wasiwasi hawatakosa korosho za kubangua,” alisema.

Alisema Serikali haitegemei kuuza korosho ghafi nje ya nchi kama viwanda vya ndani vitakuwa na uwezo wa kubangua, hivyo kabla ya kuuza kwa wanaosafirisha, wataulizwa kwanza mahitaji yao ndipo wengine watauziwa.

Waziri huyo alisema mpango huo hautaishia kwa korosho tu, bali mazao yote ya kipaumbele ambayo ni kahawa, pamba, chai, tumbaku na pareto, lengo likiwa ni kuvutia uwekezaji wa viwanda vya kuyaongezea thamani.

Kubangua

Kuhusu kubangua, Waziri Hasunga alisema lengo la Serikali ni kubangua korosho ghafi tani 50,000. Hadi sasa kuna viwanda tisa vimeingia mkataba wa kubangua tani 31,400 na Serikali inajadiliana na vingine vinavyoatarajia kuchukua tani 10,000.

Alisema korosho hizo zinazobanguliwa ni kwa ajili ya soko la ndani na nje kwa kuwa lengo ni kuuza zilizobanguliwa lakini uwezo wa viwanda vya ndani ni mdogo ndiyo sababu mwaka huu wametenga kiasi hicho kidogo.

“Kusafirisha korosho zilizobanguliwa na kuongezewa thamani kutasaidia nchi kuongeza pato lake na kupata fedha za kigeni,” alisema.

Kusajili wakulima

Waziri Hasunga alisema Serikali inaanza usajili wa wakulima ili wafahamike vizuri kwa kuwa takwimu na taarifa zao zikiwepo ni rahisi kwa taasisi za kifedha kama benki na kampuni za bima kuwahudumia.

“Kanzi data itasaidia kujua mahitaji ya mkulima, kujua pembejeo zipi na kiasi gani anahitaji kwa kuzingatia ukubwa wa mashamba yake. Hata kwa Serikali inakuwa rahisi kuwawezesha na kuwaepusha na utaratibu wa kangomba ambao ni wa kinyonyaji,” alisema Hasunga.

Alisema pamoja na hatua hiyo, Serikali inaimarisha ushirika na saccos ili wakulima wakiwa na shida au mahitaji waweze kupata mikopo na misaada.

Fedha ambazo Serikali imetumia katika Korosho

Hadi Machi 14, Serikali imeshatumia Sh599.6 bilioni. Kati ya hizo Sh576 bilioni zimetumika kuwalipa wakulima.

Waziri Hasunga alisema hadi kumaliza mchakato mzima wa malipo na gharama nyingine, Serikali inatarajia kutumia Sh723.1 bilioni.

Alisema gharama hizo nyingine ni kwa ajili ya usafirishaji, maghala, ubanguaji na ukusanyaji.

Waziri Hasunga alisema Serikali inadaiwa Sh197.6 bilioni kati ya hizo, fedha za wakulima ni Sh147 bilioni na kati ya fedha hizo za wakulima, Sh32.3 bilioni zimeshapelekwa benki lakini Sh15.5 bilioni zimeshindwa kuingia katika akaunti za wakulima kwa sababu mbalimbali.

Alisema fedha zilizobaki (Sh115 bilioni) zinasubiri kukamilika kwa uhakiki.

Chanzo: mwananchi.co.tz