Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshahara kuleta mageuzi ya uchumi

C8bb5a31c887c5d328f1fe4d9d4e9d31.jpeg Mshahara unatarajiwa kuanza Julai Mosi mwaka huu

Mon, 23 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wamesema ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma litakuwa na manufaa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi.

Walisema ongezeko hilo linatarajiwa kuingiza Shilingi trilioni 1.6 kwenye uchumi wa nchi katika mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai Mosi mwaka huu.

Hivi karibuni Rais Samia alitangaza kuridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa kima cha chini kuongezwa kwa asilimia 23.3.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh 9.7 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wa umma.

Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk Ahmed Sovu, alitaja faida sita za uamuzi wa serikali ikiwemo ya kuongeza mzunguko wa fedha kwenye jamii.

“Jamii huwa inapata fedha zake kupitia mzunguko wa wenzao wenye ajira. Kwa kuwa wao kama jamii hawana njia yoyote ya kupata hela kutoka katika mfuko wa serikali, yaani hazina moja kwa moja," alisema Dk Sovu.

Alisema kupitia ongezeko hilo watumishi wataingiza fedha kwenye mzunguko wa uchumi ikiwa ni pamoja na kutoa michango kwenye harusi, kulipa ada za shule, kuwatumia ndugu fedha za matumizi, kujenga nyumba na kununua vifaa au bidhaa.

"Ongezeko hili la mshahara linaenda kuleta faraja na kuondoa msongo wa mawazo kwa wafanyakazi wenyewe na hata familia zao. Kimsingi, ongezeko la mshahara huleta faraja kwa watumishi na wafanyakazi wao. Hivyo, hupunguza stress (Shinikizo) na kuimarisha ndoa na hatimaye huondoa migogoro ya kifamilia na kudumisha mahusiano baina ya wanandoa, watoto na hata ndugu wengine," alisema Dk Sovu.

Alisema ongezeko hilo litaongeza ari ya kazi hivyo kuongeza tija, migogoro itapungua kwenye jamii kwa kuwa mtumishi ataweza kulipa kulipa madeni ikiwemo mikopo, ada na kodi za nyumba.

"Ni muhimu kuwa na masoko ya ziada ili kuongeza kasi ya biashara na kuwa na ubunifu wa kuibua ajira mbalimbali kama vile Rais Samia Suluhu Hassan alivyobuni filamu ya "Royal Tour " ili kuchochea na kukuza utalii na kuongeza ajira kwa vijana na jamii kwa ujumla. Mambo yote haya Mheshimiwa Rais Samia ameyafanya hasa hili la kuongeza ajira mpya kila wakati linasaidia kuongeza mzunguko wa fedha kwa watu wa kawaida kwenye jamii,"alisema Dk Sovu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na Mwanasheria wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Joel Nchimbi aliishukuru serikali kwa nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma.

Nchimbi alimpongeza Rais Samia kwa kupandisha madaraja kwa watumishi wa umma, kulipa malimbikizo ya mshahara na nyongeza ya mshahara na akasema hii ni neema kwa watumishi wa umma.

Mchumi na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Vincent Stanslaus, alisema malipo ya malimbikizo ya mshahara, kupandisha daraja na ongezeko la mshahara vitaenda kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

"Makusanyo ya kodi ya serikali kutokana na manunuzi yatakayofanywa na wafanyakazi yataongezeka na pato la taifa litaimarika," alisema Stanslaus na kuongeza;

"Tanzania tumejitahidi kudhibiti mfumuko wa bei kutoka tarakimu mbili hadi tarakimu moja na mwezi uliopita mfumuko wetu wa bei ulikua ni 3.8% ambacho ni kiwango cha chini Afrika Mashariki iliyojiwekea lengo ya mfumuko wa bei wa 5%. Mfumuko huu mdogo wa bei ni mzuri kiuchumi, unachochea maendeleo na ni stahimilivu."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live