Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msako wanaouza sukari bei juu Dar kuanza leo

SUKARII.webp Msako wanaouza sukari bei juu Dar kuanza leo

Tue, 5 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuanzia leo mkoa wake utawakamata wafanyabiashara wanaouza sukari kinyume cha bei elekezi isiyozidi Sh. 2,600 kwa kilo.

Amesema katika ukaguzi wao huo, sukari itakayokamatwa inauzwa kinyume cha maelekezo ya serikali, itataifishwa huku wahusika wakikamatwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Makonda alisema amebaini baadhi ya wafanyabiashara wanauza kilo moja ya sukari kwa Sh. 3,500 badala ya Sh. 2,600 iliyoelekezwa na Wizara ya Kilimo.

Kutokana na hilo, amewaagiza wakuu wa wilaya zote tano mkoa huo kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa kuwabaini wafanyabiashara hao ili wakamatwe na sukari hiyo itaifishwe.

“Msako huu unaanza kesho (leo) na asisalie mfanyabiashara yeyote anayeuza sukari kwa bei ya juu,” aliagiza.

Makonda alisema hakuna sababu ya kutumia mwezi wa Ramadhani kuwakandamiza watu.

“Sukari yote hata ikiagizwa nje ya nchi, inapita Dar es Salaam haiwezekani mkauza mpaka Sh. 3,500 kwa kilo. Timu ya mkoa imepita, inawafahamu wafanyabiashara wote. Kuanzia kesho (leo) tutaanza kukamata wafanyabiashara na kutaifisha sukari ambayo mnauza bei juu.

“Tumewaambia kwa sababu tunawapenda ili muda huu (jana) mfanye marekebisho lakini kuanzia kesho (leo), Wakuu wa Wilaya Kigamboni, Temeke, Ilala, Kinondoni na Ubungo na timu zenu piteni, kamateni na kuichukua hiyo sukari," aliagiza.

Makonda alisema uongozi wa mkoa huo utaichukua sukari hiyo na kuiuza kwa bei elekezi na fedha itakayopatikana ikatumika kununua vifaa vya kuwakinga madaktari wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Hakuna sababu ya kupimana ubavu, kuuza nje ya maelekezo ya serikali bei inajulikana na serikali ilitoa vibali vya uagizaji nje ya nchi, hakuna sababu ya kupandisha bei na kuwaumiza wananchi,” alisema.

Mwezi uliopita, serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilitoa bei elekezi ya bidhaa hiyo muhimu. Bei hiyo inanzia Sh. 2,600 hadi 3,200 kwa kilo, ikizingatia jiografia ya mkoa husika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live