Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msako mkali kuwaondoa watoto mashamba ya vitunguu waja

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Karatu.Kamati ya ulinzi na usalama wilayani hapa ikishirikiana na viongozi wa serikali za vijiji itaendesha  msako mkali wa kuwaondoa watoto wanaotumikishwa kwenye mashamba ya vitunguu ili waendelee na masomo.

 

Mkuu wa wilaya ya Karatu mkoa wa Arusha,Theresia Mahongo amesema hayo jana katika Kijiji cha Qang'dend wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika ngazi ya wilaya na kuwataka wanaowatumikisha wache mara moja.

 

"Serikali haitavumilia kuona watoto ambao umri wao wanapaswa kuwa shuleni wanafanyishwa kazi ngumu kwenye mashamba ya vitunguu,watoto wanapaswa kufanya kazi nyepesi chini ya uangalizi wa wazazi wao na tutakaowabaini tutawachukulia hatua za kisheria,"amesema Mahongo

 

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Karatu,Felix Sulle alisema kwa kushirikiana na wadau wengine wamefanya mambo mengi ya kuwasaidia na kuwalinda watoto wafikie ndoto zao katika maisha.

 

Amesema halmashauri hiyo ilitenga kiasi cha Sh8milioni kwa ajili ya kuwanunulia vifaa vya elimu wanafunzi wanaotoka kaya masikini pia kupitia mfuko wa Tasaf familia nyingi zimewezeshwa ili kuwasaidia watoto wengi kuhudhuria darasani.

 

Naye Kaimu Mratibu wa shirika la World Vision Lake Eyasi ADP,Sitta Nyakizaza amesema wadau wa kutetea haki za watoto kwa kushirikiana na jamii wanakatishwa tamaa na vyombo vya dola vinavyoshindwa kushirikiana nao kupunguza ukatili kwa watoto.

 

Amesema yapo matukio ya watuhumiwa kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola lakini baadaye ushahidi na vielelezo hupotezwa kwa lengo la kumsaidia mtuhumiwa asitiwe hatiani jambo linaloongeza vitendo viovu.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz