Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msajili aonya fedha za miradi kufanyia matanuzi

782c62432a1a3e30116143a423fd4b8a.jpeg Msajili aonya fedha za miradi kufanyia matanuzi

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Msajili wa Bodi ya Makandarasi nchini (CRB), Rhoben Nkori, amewataka wakandarasi kuacha tabia ya kutumia fedha za miradi kufanya matanuzi kabla ya miradi hiyo kukamilika kwani wanaweza kushindwa kuitekeleza.

Alitoa angalizo hilo mwishoni mwa wiki wakati akifunga mafunzo kwa wakandarasi wazalendo wa mikoa ya Iringa, Njombe, Dar es Salaam, Mbeya, Rukwa, Dodoma, Tanga, Morogoro, Mwanza na Ruvuma iliyofanyika mkoani Iringa.

Alisema kazi ya ukandarasi ni biashara inayohitaji mipango na usimamizi wa fedha kwa kufuata maadili ya kazi ili kujenga uaminifu wa kupata kazi zingine kwa wateja wao badala ya kutumia fedha kabla ya mradi.

“Huwezi kupata faida kabla ya mradi kukamilika na ili upate faida lazima ukae kwenye ratiba uliyojiwekea na kufanyakazi kwa malengo uliyojiwekea na kuna faida kubwa kukamilisha mradi mapema kwa sababu unaokoa gharama nyingi za kulipa wafanyakazi na mashine ulizokodi,” alisema.

Aliwataka wakandarasi kuheshimu mikataba wanayoingia na wateja wao ikiwemo kuepuka matumizi ya fedha za miradi nje ya shughuli za miradi kabla ya kumaliza miradi husika.

"Unapopewa mradi uheshimu kwa sababu wengi wetu tunapewa pesa za miradi tunatumia kwa mambo yetu binafsi kabla ya mradi kuanza, jambo ambalo linasababisha wakati mwingine kupata hasara na mradi kutomalizika kwa muda na ubora uliopangwa," alisema.

Mmoja wa wakandarasi walioshiriki mkutano huo, Emmanuel Mshana kutoka Kampuni ya ukandarasi ya LABA ya Dar es Salaam, alisema mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwa wakandarasi.

"Tumejifunza namna ya kuandaa mpango kazi, kusimamia mikataba yetu na jinsi ya kutumia mfumo wa kuwasilisha zabuni kwa njia ya kielektroniki TANePS,” alisema.

Naye Osward Kikoti ambaye ni mkandarasi aliishukuru CRB kwa kuwapatia mafunzo hayo ambapo alisema kwa sasa wanajua nini cha kufanya pale wanapoingia mikataba na kukutana na changamoto mbalimbali.

"TANEPS imetusaidia kwa kiasi kikubwa kulinganisha na zamani ambapo sasa inatusaidia matumizi ya muda na kuepuka mlolongo mrefu wa kufikisha zabuni yako mahali popote pale,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz