Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa uchumi kuleta mapinduzi ya teknolojia UDSM

Uchumi Kupanda Mradi wa uchumi kuleta mapinduzi ya teknolojia UDSM

Tue, 7 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) unatarajiwa kuleta mageuzi ya teknolojia katika chuo hicho.

Pia kuzalisha wahitimu wenye uelewa na ujuzi juu ya matumizi ya teknolojia mpya ambazo kwa sasa zinatumika katika maeneo mbalimbali watakayokwenda kufanyia kazi mara baada ya kuhitimu.

Hayo yameelezwa jana Machi 6, 2023 jijini Dar es Salaam na Profesa Bakari Mwinyiwiwa kutoka katika kitivo cha katika mkutano ulioandaliwa na chuo hicho kwa ajili ya kuwajengea uelewa wakuu wa vitivo mbalimbali juu ya utekelezaji wa mradi huo.

Profesa Mwinyiwiwa amesema utekelezaji wa mradi huo pia utasaidia upatikanaji wa vifaa ambayo vitawezesha wanafunzi kujifunza matumizi ya vifaa muhimu ambayo atavikuta katika eneo la kazi.

"Tunaupokea mradi huu kwa mikono miwili kwani unakwenda kuleta maendeleo makubwa katika chuo hiki,"anasema.

Kwa upande wake Dk Magreth Kyewalyanga ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari ya chuo hicho iliyopo Zanzibar anasema utekelezaji wa mradi huo katika taasisi hiyo itasaidia kukamilishwa kwa majengo yaliyokuwa hayajakamilika katika chuo hicho pamoja na ujenzi wa hosteli za wanafunzi njirani na eneo ilipo taasisi hiyo.

"Ujenzi wa hosteli jirani na chuo utawasaidia wanafunzi kupunguza muda wanaokuwa wanatumia kutoka maeneo wanakoishi hadi kufika chuoni"

Dk Kyewalyanga anasema kukamilika kwa ujenzi wa majengo na hosteli kutawawezesha hata kufundisha programu nyingi zaidi katika taasisi hiyo.

Akizungumza na katika mkutano huo Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema lengo la mkutano huo ni kuwapa uelewa wakuu wa vitivo na vitengo mbalimbali vilivyopo chuoni hapo juu ya utekelezaji wa mradi wa HEET chuoni hapo ili kushirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wake.

Profesa Anangisye anasema mradi huo unalenga kuifanya elimu ya juu iweze kuchangia katika mageuzi ya uchumi wa nchi kwa kuwajengea uwezo wahitimu.

HEET ni mradi unaotekelezwa na Serikali chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ukilenga kuleta mapinduzi katika elimu ya juu nchini pamoja na kutolewa kwa elimu inayoendana na soko la ajira .

Chanzo: www.tanzaniaweb.live