Arusha. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametoa wito kwa taasisi za fedha kuongeza kiwango cha fedha za mikopo kwenye sekta ya ufugaji ambayo ina nafasi kubwa ya kukuza mapato ya wafugaji na kuongeza faida ya taasisi hizo.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa kitaifa iliyofanyika Juni mosi mwaka 2019, jijini hapa alisema taasisi za fedha zinatakiwa kuwa na mitazamo tofauti kuhusu sekta ya mifugo na tasnia ya maziwa kwa ujumla.
“Nitoe rai kwenu taasisi za fedha msipende kukariri kwa kuangalia maombi ya mfugaji anayetaka mkopo na kumjibu kuwa dhamana zake haziendani na kiwango cha mkopo anaotaka kuchukua, mnapaswa kubadilika na kuona fursa iliyopo kwenye soko la maziwa nchini,” alisema Mpina.
Alisema lengo la kuzitaka taasisi za fedha kuongeza utoaji wa mikopo ni kupunguza kiwango cha uagizaji wa maziwa kutoka nje kwa kuwajengea uwezo wazalishaji wa ndani kukidhi mahitaji ya soko la maziwa yaliyosindikwa.
Meneja Mahusiano na Mikopo ya Kilimo wa benki ya CRDB, Maregesi Shaaban alisema wamekua wakitoa mikopo ya viwango tofauti kwa wafugaji kwaajili ya kuboresha mnyororo wa thamani wa wafugaji na kuongeza thamani ya maziwa yanayopatikana.
“Benki yetu imejipanga kutoa elimu kwa wakopaji wetu kulingana na vipaumbele vyao ili waweze kupata matokeo yenye tija kwenye maeneo yote yenye mazao ya kimkakati nchini na kuhakikisha viwanda vyetu vinafanya kazi kwa kupata mali ghafi za kutosha,” alisema Shaaban
Pia Soma
- UREMBO: Namna sahihi ya kuondoa vinyweleo
- ANTI BETTIE: Mke wangu hajui Kiingereza, nifanyeje ananitia aibu
- Malaria tishio wilayani Rorya
- Mvutano waisha, Savimbi azikwa kando ya baba yake
Kwa upande wake Afisa Biashara na Mikopo wa benki ya Maendeleo ya Wakulima (TADB), Furaha Sichula alisema benki hiyo inatoa mikopo ili kuongeza tija kwa wafugaji katika kuwezesha upatikanaji wa mitamba bora na uongezaji tija kwenye chakula cha mifugo.
Pia amesema TADB inatoa mikopo kwaajili ya utunzaji wa maziwa na kuongeza kiwango cha usindikaji wa maziwa pamoja na usafishaji kutoka kwa wafugaji kwenda viwandani .