Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpina aagiza kiwanda kudhibiti viwango vya bei 

846ad0dfd8bcdcf542a5899e6303990b Mpina aagiza kiwanda kudhibiti viwango vya bei

Wed, 19 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amekiagiza Kiwanda cha Galaxy Food and Beverage Limited, kuhakikisha kinadhibiti viwango vya bei, ili kuondoa hujuma za kibiashara zinazofanywa na wajanja wachache na kushusha thamani ya maziwa yanayozalishwa nchini.

Akizungumza jijini Arusha juzi wakati alipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kujionea uzalishaji wa maziwa, Mpina alisema serikali imeweka mazingira rafiki ya biashara ili kuwezesha maziwa yanayozalishwa nchini kuwa na soko zuri popote yanapouzwa.

"Katika bajeti ya serikali ya mwaka huu, kupitia Wizara ya Fedha, tumeondoa tozo na kodi mbalimbali ili kuwezesha uwekezaji huu kuendelea kuleta tija na matokeo chanya hapa nchini, hivyo tozo na kodi sio tatizo tena sasa jipanueni nchi nzima hizi asilimia 70 hazitoshi fikisheni 100," alisema.

Alisema maziwa yanayozalishwa na kiwanda hicho ambayo hufahamika kwa jina la Tanga Fresh, yana ubora ambao unatakiwa huku akiwataka kupeleka bidhaa hiyo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na masoko yote ya ndani, kwa kuwa uhitaji ni mkubwa.

"Mifumo ya bei inapaswa kuangaliwa kwa ukaribu ili wauzaji maziwa kwa mawakala wauze kwa bei nafuu na hata yale ya sokoni bei iwe nzuri ili tutofautishe na maziwa yanayotoka nje ya nchi," alisema.

Mpina alikipongeza kiwanda hicho kwa kununua maziwa kwa wafugaji kwa bei inayoridhisha ya zaidi ya Sh 800 na kuzingatia kipaumbele cha serikali cha kutaka bei za bidhaa hizo ziwe nafuu.

Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Noely Byamungu alisema uwepo wa kiwanda hicho ni muhimu katika kukuza uchumi wa wafugaji na nchi.

Pia alisema kazi ya bodi hiyo ni kusimamia, kuratibu na kuendeleza tasnia ya maziwa na wafugaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wafugaji wanafuga kisasa na kuzalisha malighafi zenye ubora unaohitajika sokoni.

Hasheem Said ambaye yupo katika kitengo cha uendeshaji kiwandani hapo aliipongeza serikali kwa kuanzisha viwanda na kuvifufua vilivyokufa kwani hatua hiyo imesaidia vijana kupata ajira.

Hata hivyo, aliiomba serikali kusimamia sera ya unywaji wa maziwa, ili kuongeza idadi ya Watanzania kutumia bidhaa hiyo na kuongeza uzalishaji viwandani.

Chanzo: habarileo.co.tz