Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpango wa kuchoma mkaa kiteknolojia upo mbioni

42390 Pic+mkaa Mpango wa kuchoma mkaa kiteknolojia upo mbioni

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tatizo la uchomaji wa mkaa holela unaoharibu misitu nchini litakwisha endapo teknolojia za uchomaji mkaa itatumika.

“Hata Ulaya wanachoma mkaa, lakini kunakuwa na utaratibu maalumu ambao wachoma mkaa wanasajiliwa na wanajenga viwanda vyenye matanuru ya kisasa na kila mchoma mkaa anapouza lazima aonyeshe risiti na mkaa huo umechomwa tanuru gani,” anasema mtendaji mkuu wa kampuni ya Green Gold Treasure Tanzania (GGT) Amon Mnzava.

“Kila mchoma mkaa atumie vifungashio vyenye anuani kamili na uzito wa mkaa. Serikali siyo tu kwamba itadhibiti uchomaji wa mkaa, bali itaingiza mapato kwa kukusanya kodi,” anaongeza.

Mnzava anasema kampuni hiyo ina mkakati wa kukabiliana na uchomaji holela wa mkaa kwa kudhibiti nishati hiyo kuingia Dar es Salaam bila kuwa na vifungashio na kutojulikana umechomwa wapi na kwa namna gani.

Anasema kuna tofauti kati ya mkaa unaochomwa kienyeji na utakaochomwa kiteknolojia. Unaochomwa kienyeji una unyevu kwa asilimia tano wakati huu mwingine una asilimia tatu tu. Pia kiwango cha kaboni cha mkaa wa kiteknolojia ni asilimia 88-92 wakati wa kienyeji ni 47 hadi 50.

“Wakati mkaa wa kienyeji huungua kwa saa moja hadi mawili wakati wa matumizi, mkaa mpya unaweza kutumika kwa saa tano hadi sita na kiwango chake cha majivu ni asilimia 0.02 wakati mkaa wa kienyeji una asilimia tatu ya majivu,” anasema Mnzava.

Uwekezaji mkubwa

(GGT) ambayo ni kampuni ya ubia kati ya Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na sekta binafsi kupitia kampuni za Edosama Hardware Ltd inatarajia kuwekeza Sh52 bilioni katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya miti kwa ajili ya mbao za kisasa na mkaa mbadala.

Uwekezaji huo unakuja wakati Tanzania ikitegemea mazao ya misitu kama vyanzo vya nishati kwa asilimia 90, huku petroli ikitegemewa kwa asilimia nane na umeme asilimia mbili.

Tanzania ina eneo la hekta 48.2 milioni za misitu, sawa na asilimia 54.6 ya ardhi yote kwa mujibu wa Ripoti ya Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Misitu (Naforma) ya mwaka 2015.

Pia inaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye utajiri wa misitu ikiwa na mita za ujazo 3.3 bilioni za miti ya asili ambayo ni asilimia 97 ukiondoa miti ya kupandwa.

Hekta 27 milioni za miti hiyo ziko kwenye maeneo ya hifadhi kama mbuga za wanyama, vyanzo vya maji na hivyo hairuhusiwi kuvunwa kisheria.

Licha ya miti mingi ikitumika kuzalisha nishati kupitia mkaa na kuni, biashara ya mkaa inaingiza asilimia tatu tu ya mapato ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Kuhusu uwekezaji huo, mkurugenzi mtendaji wa Edosama Hardware, Edward Maduhu anasema viwanda hivyo vitajengwa Mafinga na Njombe na vitakuwa vikichakata miti na mabaki yake kutengeneza mkaa mbadala unaoitwa ‘Charcoal Briquetts’ na mbao mbadala aina ya MDF board, partcle board na block board.

Anasema uwekezaji huo umekuja baada ya kufanya utafiti wa kina tangu mwaka 2011 ambao bado unaendelea ili kuhakikisha njia bora za kutumia mazao ya misitu zinapatikana.

Maduhu anasema uchomaji wa mkaa unaofanywa kienyeji ndiyo chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu na kwamba njia watakayotumia itapunguza uharibifu huo kwa asilimia 80.

“Ikiwa TFS watashirikiana na wadau kama sisi tutaeneza teknolojia hii kwa kujenga matanuru maalumu ya uchomaji wa mkaa yatakayokuwa yamesajiliwa. Uchomaji huu wa mkaa unaweza kuipatia TFS ya Sh125 bilioni kwa mwaka,” anasema Maduhu.

Mkurugenzi mkuu wa NDC, Profesa Damiani Gabagambi anasema maandalizi ya ujenzi wa kiwanda hicho yanaendelea ikiwa pamoja na kupata eneo la ujenzi huko Mafinga.

“Tutakuwa na kiwanda kitakachoongeza thamani ya mti, kwa sababu kwa sasa Tanzania tunatumia asilimia 45 tu ya mti na hiyo inayobaki inatupwa. Tunataka tuongeze thamani ya mti ili kutumia hadi asilimia 98 ya mti kwa tija,” anasema Profesa Gabagambi.

Mtendaji mkuu wa wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo anasema wamekuwa wakiipa GGT msaada ili kuwezesha uwekezaji huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz