Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpango mpya kuwainua wajasiriamali huu hapa

Wajasiriamali Dom Mpango mpya kuwainua wajasiriamali huu hapa

Tue, 12 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya CRDB na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) leo Jumanne Julai 12, 2022 zimesaini mkataba utakaowawezesha mitaji wajasiriamali wadogo na wa kati kutoka Tanzania na Burundi.

Hafla ya utiaji saini mkataba huo imefanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam ambao pia unalenga kuimarisha uchumi wa nchi hizo kutokana na athari za janga la UVIKO-19.

Kupitia ushirikiano huo, IFC inatoa mkopo wa Dola za Marekani 100 milioni kwa CRDB nchini na mkopo wa dola za Marekani 5 milioni kwa CRDB Burundi.

Mkurugenzi wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela amesema fedha hizo zinalenga kuwawezesha wafanyabiashara hasa wanawake kupata mikopo.

"Fedha hizi zimekuja wakati muafaka na zitaongeza uwezo wetu wa kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati huku tukisaidia kuongeza usawa wa kijinsia katika mnyororo wa thamani.

“Tunaamini kuwa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ni msingi wa maendeleo,” alisema Nsekela.

Amesema ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili utakuza sekta ya ujasiriamali katika mataifa husika na kwamba mkataba huo ni wa tano kati ya taasisi hizo kwani zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu.

Amesema asilimia 25 ya mkopo unaolekezwa nchini utatolewa kwa biashara zinazomilikiwa na wanawake.

Tanzania ina wastani wa biashara ndogondogo na za kati milioni 3.2 ambazo kwa ujumla wake huchangia asilimia 27 ya pato la taifa na kuajiri watu milioni tano.

Hata hivyo, asilimia 81 ya biashara hizo hazina uwezo wa kupata fedha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live