Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpango mkakati wa DCB miaka mitano kujadiliwa

DCB Mpango mkakati wa DCB miaka mitano kujadiliwa

Thu, 25 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WANAHISA wa BENKI ya Biashara ya DCB wanatarajia kujadili mpango mkakati wa benki hiyo wakati wa mkutano mkuu wa mwaka unaotarajiwa kufanyika Jumamosi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfrey Ndalahwa, alisema, mkutano huo utakuwa wa kihistoria kwani ni kwa mara ya kwanza utafanyika kwa njia ya mtandao.

Akizungumzia mafanikio ya mkakati wa miaka mitano ya utendaji wa DCB, alisema wanahisa watajadili ajenda mbili ambazo ni kuelezwa gawio la mwaka, lakini kujua taarifa ya tathmini ya mkakati wa miaka mitano waliojiwekea.

“Ikumbukwe kuwa mwaka 2017, uongozi na Bodi ya Wakurugenzi iliandaa na kupitisha mpango mkakati wa miaka mitano (2018-2022) ambao ulilenga kuirejesha benki katika mstari kutoka kwenye hasara hadi faida, kuiimarisha benki ili kuiweka sawa na tayari kwa ukuaji endelevu na upanuzi,” alisema Ndalahwa na kuongeza:

“Kufikia mwisho wa mwaka 2018, benki ilikuwa imekamilisha awamu ya kwanza ya mpango huo baada ya kupata faida ya Sh. bilioni 1.6.

“Wakati tunafunga mwaka 2019, benki ilikuwa imekamilisha hatua ya pili ya mpango mkakati huo ikiwa ni uimarishaji kupitia mafanikio ya zoezi la uuzaji wa hisa stahiki kwa wanahisa na kupata Sh. bilioni 9.7 kutoka kwenye lengo la Sh. bilioni 8.9, ikiongeza mtaji wa hisa kutoka Sh. bilioni 16 mwaka 2018 hadi bilioni 25 mwaka 2019. Hisa hizi mpya ziliorodheshwa na sasa zinaendelea kuuzwa katika soko la hisa.”

Alisema kazi kubwa imefanyika katika kurudisha benki kwenye faida, ambapo kwa mwaka 2019 ulikuwa mwaka mwingine wa mafanikio makubwa, ambapo waliweza kupata faida kabla ya kodi ya Sh. bilioni 2.10. Alisema ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na 2018 ambapo faida ilikuwa Sh. bilioni 1.62.

Kwa mujibu wa Ndalahwa, uendelezo wa faida ulichochewa na ukuaji wa mizania na uboreshaji ufanisi wa kiutendaji. Jitihada hizi zilisababisha ukuaji wa asilimia 14 katika amana za wateja, ukuaji wa asilimia 11 kwa mikopo ya wateja, ukuaji wa asilimia 22 katika mapato yasiyofadhiliwa na asilimia 9 kupungua kwa gharama za uendeshaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live