Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpango atoa maagizo biashara kimataifa

6335da818435226ec9497accf9fb777d Mpango atoa maagizo biashara kimataifa

Thu, 14 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa maagizo kwa wizara na taasisi za serikali kuondoa vikwazo vya biashara ili kuongeza na kuiweka nchi tayari kuingia kwenye masoko na biashara ya nje.

Dk Mpango alisema hayo jana wakati akifunga Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyoanza Juni 28 mwaka huu.

Aliiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikae na sekta ya fedha kuangalia namna wananchi wanaweza kupata mitaji kwa ajili ya biashara na uwekezaji.

"BoT nimewaambia waboreshe upatikanaji wa mitaji ya kuanzisha biashara. Bado Watanzania hawapati fursa ya kupewa mitaji na taasisi za fedha," alisema Dk Mpango.

Alisema iwapo taasisi za fedha zitatoa mitaji kwa wananchi kuanzisha biashara, fursa nyingi zitapatikana na masoko ya bidhaa za Tanzania nje na ndani yatapatikana.

Dk Mpango alisema hadi sasa Tanzania iko chini ya asilimia 20 katika ushiriki wake kwenye masoko ya kikanda na kusema ni lazima juhudi ifanyike ili kuongeza kiwango cha mauzo nje ya nchi.

Aliiagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) watoe mafunzo na elimu kwa wananchi na wazalishaji ili kuzalisha bidhaa bora zenye viwango zitakazopata masoko ya ndani na nje.

Pia alitaka taasisi hizo zibainishe vikwazo vya biashara vyenye kero ili kuangaliwa namna ya kushughulikiwa.

Pia aliagiza kufuatilia kwa karibu kero ukiwemo urasimu na kuuondoa kwenye mazingira ya biashara ambao umetajwa kuwa kero katika biashara.

Aidha, ameitaka wizara hiyo kushirikiana na ofisi za balozi za Tanzania nje ya nchi ili kuboresha kanzidata ya kupata fursa za masoko na biashara nje ya nchi.

"Pia wekezeni kwenye teknolojia ya kidijiti na kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa wateja kwa njia rahisi ya mtandao," alisema Dk Mpango.

Dk Mpango alitoa mwito kwa wazalishaji na wafanyabiashara watoe maoni na kuzitaja taasisi za serikali ambazo ni kero ili hatua zichukuliwe kuweka vizuri mazingira ya biashara, masoko na uwekezaji.

"Nanyi wazalishaji nchini, zingatieni kuzalisha bidhaa bora na zenye mahitaji na mzalishe kwa kiwango kikubwa. Kuweni waaminifu mnapoingia kwenye mikataba ya kibiashara," alisema Dk Mpango.

Alisema serikali inachukua hatua kuondoa kero za biashara na kuvutia utalii na kuwa ushiriki wa taasisi binafsi unahitajika.

"Moja ya kero ni upatikanaji wa vifungashio, wazalishaji wanalia na hata vikipatikana bei yake ni kubwa lazima tuwe na mkakati wa kupata suluhu ya hili," alisema Dk Mpango.

Maonesho ya mwaka huu yaliyomalizika jana yameelezwa kufanya vizuri kuliko miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Latifa Khamisi, idadi ya waliotembelea maonesho hayo imeongezeka kutoka watu 227,8143 mwaka jana hadi 315,000 mwaka huu.

Alisema idadi ya kampuni zilizoshiriki imeongezeka kutoka 3,200 mwaka jana hadi 3,425 mwaka huu zikiwemo 3,200 za ndani na 225 kutoka nje ya nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live