Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto wateketeza soko Moshi, wafanyabiashara walia na Zimamoto

Soko Kuungua Moshi.png Moto wateketeza soko Moshi, wafanyabiashara walia na Zimamoto

Tue, 6 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati moto ukiteketeza soko la Mbuyuni lililopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, gari la Jeshi la Zimamoto limeshindwa kufika eneo la tukio kutokana na ubovu.

Moto huo uliodumu kwa zaidi ya saa nne umeteketeza vibanda vyote vya biashara katika soko hilo ambalo limekuwa likihudumia wakazi wa ndani na nje ya manispaa hiyo pamoja na wilaya za jirani.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema gari la Zimamoto lilishindwa kuzima moto huo kwa kuwa ni bovu.

Babu aliyefika eneo hilo, amesema wamelezimika kuomba gari kutoka kiwanda cha sukari cha TPC kukabiliana na moto huo ulioanza saa 7 usiku.

"Tunashukuru wenzetu TPC kwa kutupatia gari la zimamoto, lakini wakati wanafika moto tayari ulikuwa mkubwa na kama unavyoona soko lote limeteketea na mali zimeteketea," amesema.

Amesema watafanya tathmini na kujua chanzo cha moto huo, huku akitaka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa kuwa Serikali ipo pamoja nao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara waliofika kwenye uokoaji wamesema hawakuweza kuokoa chochote kutokana na moto kuwa mkubwa na kulikuwa hakuna msaada wa gari la zimamoto wakati moto ilipoanza.

Samwel Steven, mkazi wa Pasua Moshi amesema walipopata taarifa za soko kuungua, walipiga simu Ofisi za Jeshi la Zimamoto, lakini hawakufika kwa wakati ule na wameshindwa kuokoa chochote kutokana na moto kuwa mkubwa.

"Soko linaendelea kuteketea na mali za ndugu zetu na mama zetu zinapotea, kuna wengine wamechukua mikopo na hatujui watarejeshaje hii mikopo, hiki ni kilio.

Kwa upande wake, Jafari Said amesema ameshidwa kuokoa chochote kutokana na moto kuwa mkubwa.

"Mali zangu zimeteketea zote, hapa nilipo sina la kufanya nimekaa tu na kuduwaa, sijui nitafanyeje na baishara hizi tunafanya kwa mikopo," amesema.

Denis Tesha, mmoja wa waokoaji waliofika katika soko hilo, amesema, "Mama yetu kapoteza kibanda chake hapa, tutapata wapi fedha ya kuwapeleka watoto shule,” amesema huku akitokwa na machozi.

Naye Mama Mushka, mmoja wa wafanyabiashara hao, amesema biashara zote walizopokea jioni hakuna hata moja iliyosalia na kwamba ni maumivu makubwa kwao.

"Huu moto umeunguza mali nyingi, karibu soko lote hakuna mtu aliyebahatika kuokoa kitu. Mali zote zilizoingia sokoni jioni hakuna hata moja iliyosalia, hapa ni maumivu makubwa.

"Gari la zimamoto limekuja hapa hakuna tulichosaidiwa na gari limekuja likiwa halina hata maji. Gari limepaki tu pembeni, wangekuja na kuzima moto haya madhara makubwa hivi yasingetokea," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live