Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moto wateketeza ghala kiwanda cha Bora

Fri, 1 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vifaa na bidhaa mbalimbali ambavyo thamani yake haijajulika vimeteketea kutokana na moto uliozuka katika ghala.

Ghala hilo ni miongoni mwa maghala kadhaa yaliyopo ndani ya viunga vya kiwanda cha viatu cha Bora kilichopo Tazara jijini Dar es Salaam.

Moto huo ulioanza alfajiri ya jana uliteketeza kwa kiasi ghala hilo lililopangishwa kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi.

Mwananchi lilifika kwenye kiwanda hicho na kushuhudia juhudi za kuzima moto huo zikiendelea na kujaribu kuokoa mali zilizomo kwenye maghala yaliyopo jirani yanayotunza bidhaa mbalimbali, zikiwamo za plastiki zinazotengenezwa na kiwanda cha Bora.

Marino Machaso ambaye alikuwa mlinzi wa zamu, alieleza kuwa saa 11:00 alfajiri alianza kuona dalili za moto katika ghala hilo na kutoa taarifa kwa fundi umeme ili kuzuia athari.

“Niliona moshi halafu na harufu ya moto, nikawahi kumtafuta fundi umeme ili akate umeme hilo likafanyika lakini moto tayari ulikuwa umeshika kasi nikawataarifu wenye kiwanda na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.

Ofisa usalama wa kiwanda hicho Sylivery Buyaga, alieleza kuwa huenda matukio ya moto yanayojirudia eneo hilo ni kwa sababu ya uchakavu wa miundombinu.

“Kiwanda ni cha muda mrefu na miundombinu yake iliwekwa muda mrefu hivyo kuna uchakavu ambao tunaweza kusema unasababisha moto kuzuka, ila uchunguzi ukifanyika utaweka wazi nini chanzo cha moto huu,” alisema.

Naye mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wilaya ya Temeke, Michael Bachubila alisema walifika eneo hilo punde baada ya kupata taarifa inagwa walizipata kwa kuchelewa.

“Nitoe rai ukiona cheche tu piga simu Zimamoto tukiwahi kufika madhara yanapungua, hawa wamechelewa walianza kupambana nao kupitia kampuni waliyoingia nayo mkataba,” alisema Bachubila.

Takriban 10 ya zimamoto yalionekana eneo hilo yakizima moto huo ambao ulisababisha kutanda kwa moshi mzito.



Chanzo: mwananchi.co.tz