Dar es Salaam. Ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu alipopatikana baada ya kutekwa, mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji maarufu kama MoDewji amesema hatasahau upendo na maombi ya Watanzania na Waafrika katika tukio la kutekwa kwake.
Mo Dewji ameandika hayo leo Januari 16 katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter huku akisema ana deni kubwa kwa nchi yake ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Amesema atafuata maneno ya Imamu wake aliyewahi kusema “usimvunje moyo mtu ambaye anakutumainia”.
“Sitasahau upendo na maombi kutoka kwa Watanzania na Waafrika wenzangu wakati wa tukio la kutekwa kwangu. Nina deni kubwa kwa nchi yangu ninayoipenda na kwa Afrika. Nitafanya kila ninaloweza kufuata kile Imamu Ali alichowahi kusema ‘usimvunje moyo mtu ambaye anakutumainia’,” amesema Dewji katika Tweet hiyo aliyoiandika kwa lugha ya Kiingereza.
Dewji alitekwa na watu wasiojulikana alfajiri ya Oktoba 11 wakati akifanya mazoezi katika Hoteli ya Colosseum iliyopo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, alipatikana Oktoba 20 katika eneo la Gymkhana baada ya kudaiwa kutelekezwa na watekaji hao.
Watu 12 walikamatwa na polisi katika tukio hilo wakihusishwa na watekaji. Familia ya Dewji iliahidi kutoa Sh1 bilioni kwa mtu yeyote ambaye angetoa taarifa ambazo zingesaidia kupatikana kwa kijana wao. Hata hivyo hakuna aliyepata fedha hizo baada ya kupatikana kwake.
Soma Zaidi: Siro, Baba wa mfanyabiashara Mo Dewji wazungumza
Soma Zaidi: Alichokisema bilionea wa Tanzania Mo Dewji mitandaoni