Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amehimiza amewataka wananchi kufanya uwekezaji wa viwanda vya kuchakata samaki ili kuongeza mnyonyoro wa thamani katika sekta hiyo.
Ameyasema hayo leo jijini hapa alipokuwa akifunga mafunzo kuwajengea uwezo wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri) kutumia data zitokanazo na tafiti za uvuvi ili kuleta tija katika uchumi.
"Kwa sasa tunahamasisha watu kuanza kufungua viwanda. Hatuwezi kusafirisha samaki kwenda nje ya nchi, lazima tusafirishe minofu ambayilo imeshachakatwa kwa ajili ya matumizi ya mlaji," amesema.
"Watu wajitokeze kwa wingi kufungua viwanda kwani ndio jambo la msingi katika kutusaidia kuchakata samaki tuweze kuuza minofu," ameongeza.
Pia amebainisha kwamba sekta hiyo bado ina mchango mdogo katika pato la Taifa ikichangia takriban asilimia zisizozidi saba.
"Mchango ni mdogo sababu data hazijaboreshwa, ndiyo maana tuko hapa kwenye mafunzo kwa lengo la kupata uelewa wa namna ya kuzitumia data kuleta tija," amesema Mnyeti.
Aidha amewataka waliopatiwa mafunzo hayo kuwa walimu wa wengine ili elimu hiyo iwe na manufaa kwa taifa zima.
Mtafiti na Kaimu Mkurugenzi wa Utafati na Uratibu, Dk Mary Kishe amesema mafunzo hayo yaliangazia mambo makuu makubwa ikiwemo namna ambavyo takwimu za kitafiti zitakavyosaidia uendelevu wa rasilimali za uvuvi.
"Pia tumeangazia ni namna gani tunaweza kuwashirikisha watunga sera na wale ambao wanasiamamia rasilimali za uvuvi," amesema Dk Mary.
Dk Mary ameongeza kuwa wameangazia namna ambavyo takwimu zinatoa uhalisia wa mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa Taifa.
"Tumegundua baadhi ya mapungufu na tumeyabainisha na tumeona umuhimu wa kuziba mapungufu hayo lakini pia fursa ambazo zipo kwenye sekta ya uvuvi," amesema.
Aidha amesema wamefanikiwa kuwaonyesha washirika walioandaa mafunzo hayo, Shirika la Chakula na Kilimo (Fao) na Chuo Kikuu cha Duke cha nchini Uingereza takwimu zilizopo na umuhimu wake.
"Tunashukuru wenzetu wa Duke na Fao kwa kujitolea kuandaa mchakato mpya wa kuangalia mchango wa uvuvi hasa kwa wavuvi wadogo," amesema.
Ofisa Uvuvi Mkuu wa Wizara ya Mifungo na Uvuvi, Lilian Ibengwe amesema walianza kufanya kazi na Fao tangu 2017 ambapo waliingia makubaliano ya kutekeleza mradi mdogo unaolenga kutengeneza mpango kazi wa kitaifa utakaoainisha changamoto za wavuvi wadogo, kuanzisha jukwaa la kina mama wavuvi na kuanzisha dawati la jenda wizarani.
"Hayo yote tulifanikiwa kutekeleza na ndipo Fao walipoamua kufanya kazi na Tanzania na tukachaguliwa kuwa miongoni mwa nchi duniani zitakazoangazia mchango wa wavuvi wadogo," amesema Ibengwe.
Amesema Fao waliamua kufanya kazi na Tafiri ili kubainisha taarifa zaidi kuhusu mchango wa uvuvi, uchakataji na uuzaji wa mazao ya uvuvi.
Pia amesema kupitia mafunzo hayo yaliyotokewa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Duke na Fao, Taifa litaweza kufahamu mchango wa sekta ya uvuvi kwa kuangalia maeneo hayo matatu.
Amesema lengo kuu ilikuwa ni kuwafundisha wataalamu wa Tafiri namna ya kukusanya taarifa za uvuvi kwenye maziwa makuu na kufahamu ni namna gani taarifa hizo zitasaidia kujua idadi ya viumbe hai ndani ya maziwa na bahari.
"Mafunzo haya yatawaisaidia namna ya kupata data kamili, namna ya kuzitunza, kuziandaa na kuzitumia ili ziweze kuleta mchango katika uchumi wa Taifa letu," amesem a Ibengwe.