Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mnada wa kimataifa wa Pugu kukarabatiwa      

D884f18bed9ca39e523a1c5a037e5330 Mnada wa kimataifa wa Pugu kukarabatiwa      

Thu, 15 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2021/22 kwa ajili ya kukarabati mnada wa kimataifa wa mifugo wa Pugu ili kuongeza maduhuli ya serikali.

Naibu Waziri wa Mifugo, Abdallah Ulega alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa (CCM) aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kukarabati mnada huo ambao ni chanzo kikubwa cha mapato ya serikali.

Ulega alisema kwa sasa serikali itakuwa inafanya ukarabati mdogo mdogo kwa kutumia fedha kidogo zilizopo wakati ikisubiri fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa mnada huo.

Akijibu swali la Mbunge Viti Maalumu, Esther Matiko (Chadema) aliyetaka kujua ni lini mnada wa mifugo wa Magena uliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime utafunguliwa kama ambavyo serikali iliahidi mwaka 2016, Ulega alisema mnada huo ulikamilika kujengwa mwaka 1995 na ulifunguliwa mwaka 1996, ambapo ng’ombe 104,000 waliuzwa na Sh milioni 260 zilikusanywa kama maduhuli ya serikali.

“Hata hivyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara mwaka 1997 iliagiza mnada ufungwe kutokana na changamoto zilizojitokeza ikiwamo wizi wa mifugo na sababu za kiusalama,” alisema.

Alisema uongozi wa mkoa wa Mara uliwasilisha ombi rasmi wizarani la kufuta mnada wa Magena na kupendekeza uhamishiwe eneo la Kirumi Check Point.

Ulega alisema wizara hiyo ilijenga mnada wa Kirumiwa Mpakani kwa gharama ya Sh milioni 321.3 na ulifunguliwa rasmi Oktoba 16, 2018.

Alisema tangu mradi huo uanze kufanya kazi, jumla ya ng’ombe 34,855, mbuzi na kondoo 5,808 wameingia mnadani hapo na Sh milioni 428.9 zimekusanywa kama maduhuli ya serikali.

Naibu Waziri huyo alisema kwa kuzingatia maoni kutoka mamlaka za mkoa, wizara itakuwa tayari kuurejesha mnada wa Magena kwa kufuata taratibu za uanzishwaji upya wa minada na kwa mujibu wa Sheria ya Nyama Na. 10 ya mwaka 2006.

Chanzo: www.habarileo.co.tz