Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlolongo wa usajili laini za simu za mkononi wawaibua polisi, TCRA

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. “Mambo kwenda holela ni kitu hatari.” Hicho ndicho alichosema msemaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala alipoulizwa kuhusu mlolongo wa usajili wa laini za simu za mkononi.

Mwakyanjala aliyasema hayo baada ya wananchi kulalamikia mlolongo mrefu wa usajili wa laini hizo pindi wanapozipoteza na kuhitaji kuzirudisha.

“Mtu anachukua namba yako halafu anasema ni yake, kisha anaichukua na kuifanyia mambo mengine,” alisema Mwakyanjala akielezea madhara iwapo usajili hautafanyika kwa umakini.

Alisema mtu anayepoteza laini ni lazima awe na vielelezo vinavyomtambulisha na kujulikana kuwa ndiye mmiliki halali.

Mwaka 2010, Bunge lilipitisha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca) ili kusimamia uuzaji, usajili na matumizi ya laini za simu za mkononi ambazo kwa Kiingereza zinaitwa subscriber identification module (Sim) maarufu kama simcard.

Kingine kilichoifanya Serikali kuweka mlolongo huo wakati wa usajili ni kuzuia uhalifu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema mtu anapopoteza laini au simu yenyewe kitu cha kwanza ni kutoa taarifa kituo cha polisi. “Inapendekezwa unapopoteza simcard yako au simu kwenye mazingira yoyote yale utoe taarifa polisi ili waweze kupeleleza isije kufanyiwa uhalifu,” alisema Mambosasa.

Alisema baadhi ya watu wanatumia mbinu za kuiba simu na kuzifanyia uhalifu na polisi wanapofanya uchunguzi mmiliki ndiye hukamatwa.

Kampuni za simu

Mkurugenzi wa mawasiliano wa kampuni ya Vodacom, Roselynn Mworia alisema anachotakiwa kufanya mtu ni kuthibitisha kama laini ni yake kwa kuwa na nakala ya kitambulisho, barua kutoka polisi na kumbukumbu ya namba angalau tatu au tano alizoongea nazo.

“Taratibu tunazotumia ni za kawaida za kuthibitisha uhalali wako ili usipewe namba ya mtu mwingine lazima uwe na barua ya polisi (ya kupotelewa-loss report), kopi ya kitambulisho chako na kumbukumbu ya namba ulizokuwa unawasiliana nazo angalau tatu au tano,” alisema Mworia.

Alisema taratibu wanazotumia ni za kawaida kama mtu anapopoteza kitambulisho kingine chochote na lengo ni kumlinda mteja wao.

Wasemavyo watumiaji

Kwa upande wao, baadhi ya watumiaji wa simu za mkononi wameonyeshwa kukerwa na mlolongo wa namna ya kurudisha laini za simu wakiziomba kampuni hizo na nyingine za mawasiliano kutafuta njia rahisi.

Mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, Joachim Simon aliliambia gazeti hili kuwa usumbufu wanaoupata ni mkubwa. “Tunapata usumbufu mkubwa sana ikiwemo kwenda polisi na huko polisi tunalipia Sh1,500 na bado laini tunanunua, tunaomba utaratibu urudishwe kama zamani,” alisema Joachim.

Rebman Malisa alisema tatizo alilowahi kukumbana nalo wakati wa kurudisha laini ni pamoja na kuulizwa namba za watu aliokuwa akiwasiliana nao ilhali alikuwa hawakumbuki.

“Mtu umepoteza laini na simu unakwenda kurudisha unaulizwa namba tano ulizokuwa ukiwasiliana nazo wakati mtu umepoteza utazitoa wapi?” alihoji Malisa.

Chanzo: mwananchi.co.tz