Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlipuko bei za bidhaa Zanzibar wamkera Dk.Mwinyi

Ef97b44d4bc4dff0c2d40757113f14be.png Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Tue, 1 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Zanzibar imesema wao si sababu ya kupanda kwa bei za vyakula visiwani humo na kwamba yupo tayari kukutana na wafanyabiashara kuangalia namna ya kupunguza bei.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema hayo jana Ikulu, Zanzibar. Dk Mwinyi alisema bei za vyakula zimepanda kwa sababu ya ongezeko la bei katika sehemu vinakozalishwa na pia ongezeko la gharama za usafirishaji na si kwa sababu ya ushuru au serikali haitaki kupunguza bei.

“Hakuna serikali inayopenda wananchi wake wawe na gharama kubwa ya maisha kwa kupandisha bei za vyakula, kwa sababu Zanzibar tunaagiza kila kitu, bei ya vyakula kule vinakozalishwa imepanda.

Wakati tani ya sukari iliyokuwa inanunuliwa Dola 400 sasa hivi tani hiyo nchini Brazil ni Dola 700, lakini mbaya zaidi ni kwamba usafiri umepanda sana, kontena lilikuwa linasafirishwa kutoka China mpaka Zanzibar hapa kwa Dola 3,500 leo hadi Dola 16,000 kwa kontena moja,” alisema.

Dk Mwinyi alisema kupanda kwa bei za vyakula liko nje ya uwezo wa mikono ya serikali kwa kuwa zimepanda zinakotoka na wakati sukari ilipouzwa Sh 2,000 kwa kilo bei ilikuwa Dola 400 kwa tani lakini kwa sasa ni Dola 700.

Pamoja na changamoto hiyo ya kupanda kwa bei, alisema serikali yake haijafunga mikono na kuacha tu bei zipande, bali imeweka bei elekezi kwamba sukari isizidi kiwango fulani. Alisema amekubali ombi la wafanyabiashara la kutaka waonane naye ili kulipatia ufumbuzi suala la bei za vyakula ukiwemo mchele na sukari.

“Tunaweza kutazama kushusha kodi tulizonazo, lakini tuangalie sukari inatoka wapi kwa mfano, nimepewa taarifa kuna sukari ya jirani hapa Msumbiji, Uganda, Zambia lakini watu bado wanataka kununua sukari ya Brazil, kutoka Brazil mpaka hapa usafiri bei kubwa sana na sukari yenyewe imeshakuwa bei kubwa, kwa hiyo tutazame hili la sukari ya karibu hapa kama itatuwezesha kuuza kwa bei nzuri kabla ya kupunguza ushuru,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema serikali itasimamia ili vyakula visiendelee kupanda bei ikiwemo kuweka bei elekezi ili wafanyabiashara wasipandishe bei wanavyotaka wao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live