Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlima huu wa tozo wawaliza wenye mabasi, malori

Malori 0 Mlima huu wa tozo wawaliza wenye mabasi, malori

Fri, 17 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Serikali ikipanga kuanza kutoza kodi ya Sh3.5 milioni kwa kila lori la mizigo na basi la abiria kwa mwaka, wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri wameomba kiwango hicho kipunguzwe.

Pia, wameomba ufanyike uchambuzi wa kina kuonyesha gari linalopaswa kulipa fedha hizo kwa kuwa magari yanatofautiana uwezo.

Ushauri huo umetolewa jana, siku moja tangu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kutangaza azma hiyo aliposoma bajeti kuu ya mwaka 2022/23.

Mwigulu alisema kodi hiyo inakusudia kuongeza mapato ya Serikali, hivyo kuiwezesha kutekeleza majukumu ya kuihudumia jamii.

“Kodi hiyo inatarajiwa kuiongezea Serikali Sh141.05 bilioni,” alisema Dk Mwigulu.

Akiizungumzia kodi hiyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus John alisema ni vyema Serikali ikaipunguza walau iwe Sh2 milioni ili kuwaondolea mzigo wa uendeshaji wamiliki wa mabasi.

“Japokuwa njia hii ni nzuri kukusanya mapato ya Serikali na itawawezesha wamiliki kulipa kodi mara moja na kuachana na Serikali, lakini kiasi hicho kipunguzwe kitawaumiza watu. Wapo watu wanaomiliki zaidi ya mabasi 100,” alisema John.

“Mabasi ya abiria na malori ya mizigo yanatofautiana uwezo, mfano Coaster, Fuso, lori, Hiace na semitrailer, basi wamiliki waeleweshwe kiasi wanachostahili kulipa kulingana na gari ambalo kila mmoja analo.”

Awali, alisema ulipaji kodi hizo ulikuwa ukifanyika kwa namna mbili, kwanza ni gari ambalo mapato yake yalikuwa hayajafika Sh100 milioni kwa mwaka na ililipwa Sh800,000 hadi Sh1.5 milioni.

“Kwa yale yaliyozidi Sh100 milioni, mtu alilipa asilimia 30 ya faida aliyoipata ndani ya mwaka mzima. Namna ya ulipaji tu imebadilishwa lakini kodi ilikuwepo,” alisema John.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay alisema wazo hilo ni zuri, lakini ni vyema Serikali iangalie namna ya kuipunguza kodi hiyo iwe kati ya Sh1.5 milioni na Sh2 milioni.

“Sisi tulikuwa na mapendekezo ili watu waweze kulipa kodi kwa hiari na tukapendekeza iwe kati ya Sh1.5 milioni na Sh2 milioni, lakini Serikali imeenda mbali zaidi, tumeipokea, ni sehemu nzuri ya kuanzia, lakini ni vyema ikapunguzwa hadi tulipopendekeza,” alisema Lukumay.

Takwimu zinaonyesha wanachama wa Tatoa wanamiliki zaidi ya malori 60,000 yanayosafirisha mizigo ndani na nje ya nchi.

Kodi ya mafuta

Ukiacha kodi hiyo itakayotozwa kwenye malori na mabasi, Serikali imeanzisha kodi ya Sh20 kwa kila mafuta atakayotozwa muuzaji wa rejareja wa dizeli, petroli na mafuta ya taa.

Mapato ya kodi hiyo, Dk Mwigulu alisema yatakusanywa na wauzaji wakubwa wa nishati hiyo, hivyo kuirahisishia Serikali jinsi ya kuyapata badala ya kuzunguka kwenye vituo vyote vya mafuta nchini ambavyo Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo alisema vipo zaidi ya 2,000.

Kuhusu utaratibu huo, Waziri Nchemba alisema utarahisisha ulipaji kodi wa vituo vya mafuta na kupunguza gharama za matumizi, hasa karatasi za kutolea risiti za kielektroniki na Serikali itapata Sh59.82 bilioni kwa kodi hiyo.

Akizungumzia kodi hiyo, John wa Taboa yenye mabasi 8,000 ingawa yanayofanya kazi ni 5,400 alisema itaongeza gharama za uendeshaji, licha ya Serikali kuchukua hatua kadhaa za kushusha bei ya mafuta nchini, ikiwamo kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni kila mwezi.

Hata hivyo, Lukumay wa Tatoa alisema kodi hiyo itaongeza gharama za uendeshaji kwa sasa, lakini baadaye itakuwa na manufaa katika kuzuia kupanda kwa mafuta.

Taarifa zinaonyesha Tanzania inatumia wastani wa lita milioni 10 kila siku yanayouzwa kwenye vituo hivyo zaidi ya 2,000 vilivyopo nchini kote, hivyo Serikali kuwa na uhakika wa kuingiza Sh200 milioni kila siku, sawa na Sh6 bilioni kila mwezi.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Mafuta Tanzania (Tapsoa), Tinno Mmasi alisema Serikali imetoa ruzuku ili kupunguza bei ya mafuta nchini, lakini kodi hii mpya itambana mfanyabiashara atakayelazimika kupandisha bei, hivyo Serikali iliangalie kwa umakini suala hili.

“Kwa mfanyabiashara aliyekuwa ananunua lita milioni moja, maana yake anatakiwa kulipa Sh20 milioni kwanza ndipo alipie hayo mafuta. Huku ni kuua biashara ya vituo vya mafuta. Sijui kwa nini Serikali imeiweka kodi hiyo kwa wauzaji wadogo tu ikawaacha wauzaji wakubwa wakati wote wanaingia kwenye mnyororo mmoja wa thamani ya bidhaa hii,” alisema Mmasi.

Alisema kodi hiyo itaathiri biashara yao kwa kiasi kikubwa kwa kuwa inatozwa kabla mfanyabiashara hajapata faida, mtaji wake unaweza kufa kama akipata hasara.

“Kwa kawaida kodi ya mapato hulipwa baada ya kuondoa gharama zote za uendeshaji. Serikali inachukua Sh30 na mfanyabiashara anabakiwa na Sh70 kwa kila faida ya Sh100 inayopatikana, hii kodi inayopendekezwa ni mpya na itatuumiza. Naiomba Serikali iiondoe, isiwepo kabisa,” alipendekeza Mmasi.

Alisema sio wao tu watakaoumizwa na kodi hiyo, bali hata wamiliki wa mabasi ya abiria na malori ya mizigo nao watalipa zaidi hivyo kulazimika kupandisha nauli ya usafirishaji.

“Mwisho wa siku mwananchi ndiye atakayeilipa kodi hii,” alisema Mmasi.

Dereva wa daladala jijini Dar es Salaam, Michael Mwela alisema bado hajaelewa malengo ya kodi hiyo kwa kuwa miezi michache iliyopita kulikuwa na kilio cha bei kubwa ya mafuta; na hata Serikali ikalazimika kufuta baadhi ya tozo ili kumpa mwananchi unafuu wa maisha.

“Nauli zimepanda muda mfupi tu uliopita, hata baadhi ya abiria hawajazizoe. Hii kodi mpya naona itaturudisha kulekule,” alisema Mwela.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live