Mkutano wa kimataifa wa jukwaa la kiuchumi duniani unaofanyika kila mwaka umeanza leo huko Davos nchini Uswisi.
Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Oxfam limesema kuwa, makampuni ya chakula yanayotengeneza faida kubwa katika kipindi ambacho kunashuhudiwa ongezeko la mfumko wa bei yanapaswa kutozwa viwango vikubwa vya kodi ili kusaidia kupunguza ukosefu wa usawa duniani.
Hilo ni moja ya mapendekezo ya shirika hilo la msaada la kimataifa la Oxfam iliyoyatoa kwenye ripoti yake. Kwa miongo shirika hilo limekuwa likizungumzia ukosefu wa usawa katika jukwaa hilo la viongozi wa kisiasa na kibiashara huko Davos.
Mkutano huo unafanyika huku ulimwengu ukikabiliwa na matatizo mengi kuanzia mabadiliko ya tabia nchi, kupanda kwa gharama za maisha, vita nchini Ukraine taathira hasi kwa uchuumi zilizotokana na janga la Uviko-19 lakini matajiri wa dunia wameendelea kutajirika na makampuni yanazidi kuingiza faida.
Wakati huo huo Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amefutilia mbali mpango ya kuhudhuria kongamano la kiuchumi duniani mjini Davos kwa sababu ya mzozo wa nishati unaoiathiri nchi yake
Afrika Kusini inakumbwa na hali isiyo ya kawaida ya kukatika kwa umeme katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kutokana na matatizo kwenye kampuni ya serikali ya umeme ya Eskom.
Ramaphosa alitarajiwa kuongoza ujumbe wa serikali kwenye mkutano huo mkubwa wa kiuchumi, lakini badala yake amebaki nyumbani kufanya mazungumzo na Eskom na viongozi wa kisiasa ili kuangalia namna ya kulipatia ufumbuzi tatizo la uhaba wa umeme.