Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkutano wa China, Afrika waja

5913 AUGUSTINE MAHIGA Latest TZW

Fri, 6 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

TANZANIA ni kati ya nchi zitakazoshiriki mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliopewa jina la ‘Ukanda mmoja, njia moja utakaofanyika Septemba mwaka huu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema hayo jana katika maadhimisho ya kumbukumbu ya mashujaa wa China waliopoteza maisha wakijenga reli ya Tazara. Maadhiimisho hayo yamefanyika jana jijini Dar es Salaam makaburi ya Wachina Gongo la Mboto, Kambi ya Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) yakiratibiwa na taasisi ya Tanzania -China Friendship Promotion Association chini ya Mwenyekiti wake, Dk Salim Ahmed Salim kwa kushirikiana na ubalozi wa China nchini. Waziri Mahiga alisema hiyo ni fursa pekee kwa Tanzania kujitangaza kimataifa kwani mkutano huo unafungua milango katika nyanja za elimu, uchumi na kijamii na utanufaisha si tu Tanzania bali pia nchi za kiafrika kwa ujumla.

“Ukanda mmoja, njia moja, Tanzania ina nafasi kuwa kiunganishi wa nchi sita zinazotuzunguka, hivyo tunahitaji upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, reli, viwanja vya ndege na barabara kama kiunganishi, ni fursa nzuri kutumia nafasi ya mkutano huu utakaofungua milango ya nchi za Afrika kupiga hatua za maendeleo,” alisema. Pia maonesho ya uagizaji na uuzaji wa bidhaa yatakayofanyika Shanghai yametajwa kuwa yatatoa fursa kwa nchi za Afrika kuonesha bidhaa zao na kutafuta soko nchini China. Maiga alisema walipojenga reli ya Tazara, Wachina 70 walifariki kwa sababu za kuuliwa na wanyama wakali, wadudu na hali ya hewa.

Alisema urafiki uliopo uliunganishwa na damu ya Wachina waliopoteza maisha, kupata vilema vya maisha wakati wa ujenzi wa reli hiyo. “Hata Rais wa China, Xi Jinping alipoingia madarakani, kwa Afrika alitembelea Tanzania mara ya kwanza mwaka 2013, na mara ya pili alitembelea Afrika Kusini mwaka 2015. Alipokuja Tanzania alisema moyo uliooneshwa na nchi yake wakati wa kujenga Reli ya Tazara unapaswa kuendelezwa,” alisema na kufafanua, “Alichokuwa akimaanisha ni kuhusu kupanua ushirikiano wa kiuchumi baina ya China na Afrika kwa kuzingatia kila upande unufaike.”

Balozi wa China nchini, Wang Ke alisema taifa la China linaikumbuka Tazara kama moja ya miradi yao mikubwa Afrika na ya kujivunia. “Tazara inajulikana duniani kama reli ya uhuru na urafiki, nusu karne iliyopita, Wachina 50,000 wafanyakazi na mainjinia waliungana na dada na kaka zao wa Tanzania na Zambia, walifanya ujenzi wa reli hiyo katika mazingira magumu. “Kutokana na mazingira hayo, Wachina 70 walipoteza maisha. Kuwaenzi tunawakumbuka kila mwaka kwa kuwapa heshima ya kipekee. Urafiki wa Tanzania, Zambia na China umeunganishwa na damu na utaishi maisha ya Wachina daima dumu kizazi na hata kizazi. “China tunauchukulia mradi huu kama moja ya alama ya uhusiano wa kindugu baina yetu na bara la Afrika.

“Hii ni reli iliyokuwa inahitajika sana wakati huo kati ya Tanzania na Zambia ili kupambana na kero za makaburu waliokuwa wakitawala Afrika Kusini, hususani kusafirisha mizigo ya Zambia ambayo haipakani na bahari.” Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku akitoa historia ya reli hiyo alisema, “Kilichotokea ni kwamba Wachina, chini ya mwasisi wa taifa lao, Mwenyekiti Mao Zedong, walikubali kuijenga katika kipindi ambacho uchumi wao ulikuwa bado mdogo sana kulinganisha na ulivyo sasa.

Waziri wa Sheria na Katiba, Paramagamba Kabudi alisema, “China ni marafiki wa kweli kwenye shida na raha kwa nchi za Afrika, Tanzania imenufaika na China kwani walitujengea viwanda, Keko Phamaceutical, kiwanda cha UFI, kiwanda cha Urafiki, achilia mbali miradi mbali mbali ambayo walitusaidia na wanaendelea kutusaidia. Yote hiyo ni alama nzuri ya urafiki uliojengwa na waasisi wetu, ambao unadumu kizazi na kizazi.”

Tukio hilo la kumbukumbu ya maombolezo ya mashujaa wa China lilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa wizara, taasisi na idara mbali mbali za serikali, wakiongozwa na bendi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi ‘Brass band’ iliyoimba nyimbo za taifa za mataifa yote mawili kabla ya Waziri Maige na Balozi Wang kushika riboni yenye maneno ya kishujaa ya kumbukumbu.

Chanzo: habarileo.co.tz