WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa iliyopo katika biashara ya hewa ukaa.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam leo na Mwendeshaji Mkuu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya ADAP, Yves Huasser alipokuwa akizungumzia kuhusu kongamano kubwa linalotarajiwa kufanyika Dar es Salaam, Novemba 16, 2023 kwenye Hoteli ya Hyatt Regency.
“Ni biashara nzuri ambayo inaweza kuwasaidia wananchi katika maeneo mbalimbali vijijini, lakini pia inasaidia kuboresha mazingira ambayo yanaharibiwa na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Huasser.
Amesema kongamano hilo litashirikisha wadau kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Marekani na Ulaya na kwamba utakuwa mkutano mkubwa wa aina yake wenye lengo la kuwajengea uwezo pia wadau kuhusu biasshara ya hewa ukaa.
Naye Meneja Uendeshaji wa taasisi ya Africa Carbon Agency, Cosmas Tungaraza amesema kupitia kongamano hilo masuala mbalimbali yatazungumzwa na wadau wataelewa kwa undani zaidi kuhusu biashara ya hewa ukaa.
“Fursa ya hewa ukaa zina manufaa kwa jamii na serikali kwa ujumla, ndiyo maana tunalenga kuwajengea uwezo wataalamu kuhusu mambo haya ya biashara ya hewa ukaa na miradi mingine ya kaboni,lengo ni kupunguza kama sio kuondoa kabisa hewa chafu angani,” amesema.