Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi UBA asifu uwekezaji umeme wa Rufiji

64745 UBA+PIC

Fri, 28 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya UBA, Usman Isiaka amesema mradi wa kufua umeme wa Rufiji (Stiegler’s Gorge) umefanyiwa tathmini za kitaalamu na utakapokamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa.

Alisema hayo jana alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata Relini jijini hapa.

Aprili mwaka huu, UBA na CRDB walitoa dhamana ya Sh1.7 trilioni (Dola737.5 milioni) sawa na asilimia 15 ya mradi huo kwa mkandarasi anayejenga bwawa hilo ambaye ni Arab Contractors.

“Mradi umefanyiwa tathmini ya kitaalamu. Gharama zake ni halisi na hazitazidi, ndiyo maana tumekubali kutoa fedha. UBA ndiyo mkopeshaji mkubwa wa miradi ya umeme nchini Nigeria ambako benki ina zaidi ya nusu ya matawi 1,000 iliyonayo,” alisema Isiaka.

Mradi huo utakaojengwa kwa miezi 42 yakiwamo maandalizi yake, una thamani ya Sh6.6 trilioni na ulihitaji dhamana ya fedha za ndani kwa asilimia 30 na fedha za nje asilimia 70.

Mkurugenzi huyo pia alipongeza mchango wa vyombo vya habari katika kuimarisha matumizi ya huduma za fedha na kuhamasisha maendeleo ya Taifa.

Pia Soma

Licha ya mikakati mingi inayofanywa na taasisi za fedha pamoja na mipango ya Serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake, alisema vyombo vya habari vikiwaelimisha na kuwahamasisha wananchi, watashiriki na mafanikio yatakuwa makubwa zaidi.

“Tunatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari kukuza na kuhamasisha matumizi ya huduma za fedha. Benki ya UBA tunaamini huduma bora kwa wateja wetu ndicho kitu muhimu kitakachotutofautisha na washindani wetu,” alisema Isiaka.

Pamoja na kushirikiana na Serikali kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo, mkurugenzi huyo alisema wataendelea kuwahudumia wateja kwa viwango vya kimataifa. Benki hiyo iliyoanzishwa Nigeria mwaka 1949, ina matawi manne Tanzania, lakini Isiaka anaamini upo uwezekano mkubwa wa kuwafikia wananchi wengi zaidi bila kujali mahali walipo kupitia huduma zake za kidigitali.

Kupitia simu ya mkononi, alisema mteja anaweza kufungua akaunti ya akiba yenye uwezo wa kutunza mpaka Sh2 milioni na kuruhusiwa kuchukua mpaka Sh250,000 kwa siku.

Kufungua akaunti kwa simu ya mkononi, alisema mteja anatakiwa kubofya *150*70# na kufuata maelekezo yatakayofuata. Huduma hiyo inapatikana kwa wateja wanaotumia simu za mkononi.

Mkuu wa idara ya masoko na uhusiano wa benki hiyo, Brendansia Kileo alisema kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya benki kwenda akaunti ya simu ni bure Mkurugenzi huyo akiwa na watendaji wenzake walizungumza na menejimenti ya MCL masuala tofauti.

Meneja wa fedha wa MCL, Paul Ongoma alisema wataendelea kutekeleza wajibu wao wa kuwaelimisha wananchi na kuwapa taarifa za uhakika ili kuchangia maendeleo na kuboresha maisha.

“Vyombo vya habari ni mhimili wa nne, sisi tutaendelea kutoa habari za uhakika kwa wadau wote. Tunatambua uwepo wa vyanzo visivyo vya uhakika,” alisema Ongoma.

Chanzo: mwananchi.co.tz