Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkumbo ataka mifumo bora TIC, kuvutia uwekezaji

997c7957440e062425b7bce9a81408a7 Mkumbo ataka mifumo bora TIC, kuvutia uwekezaji

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, ameagiza watendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuhamasisha na kuvutia wawekezaji kwa kuboresha mifumo ya taarifa za uwekezaji kupitia njia mbalimbali ikiwemo majarida ya uchumi ya kimataifa.

Profesa Mkumbo alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TIC, alipofanya ziara ya kikazi kujionea shughuli za kiutendaji katika kituo hicho.

Alisema amegundua watu wengi hawana taarifa za kutosha kuhusu uwekezaji Tanzania, hivyo TIC waboreshe mifumo yao ya taarifa haraka.

“Katika kipindi kifupi nimegundua kuna madalali wa uwekezaji… Boresheni taarifa ili wawekezaji wajue hatua zote za kufuata katika uwekezaji Tanzania na ikiwezekana hawa madalali wasajiliwe ili kuepusha wawekezaji kutapeliwa,” alisema.

Alisisitiza TIC kuhakikisha wanatengeneza mazingira ya kujitangaza ndani na nje ya nchi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mtandao wa TIC, vyombo vya kimataifa na majarida ya kiuchumi.

“Nimegundua taarifa nyingi kwenye mtandao hazipo. Ripoti ya uwekezaji iliyopo katika mtandao wa Umoja wa Mataifa ni ya mwaka 2018, lakini iliyopo kwenye mtandao wa TIC ni ya mwaka 2016 lakini pia hamjasajili kwenye majarida ya kimataifa ya uwekezaji,” alisema.

Alisema Tanzania sasa inataka wawekezaji kutoka duniani hivyo TIC ina wajibu wa kuwahakikishia wawekezaji kwamba Tanzania ni nchi salama kwa uwekezaji tofauti na namna baadhi ya vyombo vya kimataifa vinavyoonesha nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa si sehemu salama ya uwekezaji hali inayosababisha wawekezaji wengine kuona hata nchi nyingine za Afrika si salama.

Alisema Tanzania ipo katika nchi 10 bora zinazovutia uwekezaji, lakini hiyo haitoshi kuridhika kwani Tanzania inapaswa kuwa moja ya nchi zinazoongoza kwa kuvutia uwekezaji.

“Silaha ya uchumi duniani ni kuboresha uwekezaji kwa hiyo lazima tuboreshe mazingira ikiwa ni pamoja na kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kukamilisha taratibu za uwekezaji ndani ya siku 14,” alisema.

Profesa Mkumbo alitaka kituo hicho kuwasilisha ripoti ya maendeleo ya uwekezaji nchini kila baada ya miezi mitatu na kuimarisha uhusiano na wadau wengine wa uwekezaji kama TRA na NEMC ili kuboresha mazingira na kuvutia uwekezaji.

Chanzo: habarileo.co.tz