Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkumbo:Wakulima wa ngano jiungeni kwenye ushirika

6947b1f5050896fffb3710350f64cc3e Mkumbo:Wakulima wa ngano jiungeni kwenye ushirika

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo amewataka wakulima wa ngano kujiunga katika ushirika ili kulizalisha kwa wingi na kuuza kwenye viwanda vya nchini, badala ya viwanda kuagiza malighafi hiyo nje ya nchi.

Profesa Mkumbo alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea moja ya viwanda vya Kampuni ya Said Salim Bakhresa kilichopo Buguruni na kujionea uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Sambamba na kiwanda hicho, waziri huyo alikwenda Kiwanda cha Knauf Gypsum Tanzania kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani kinachozalisha jasi na unga wake na kuridhishwa na uwekezaji wake ambao umeanza miaka mitatu iliyopita ukisubiriwa kuzinduliwa rasmi.

Akizungumza baada ya kutembelea maeneo ya uzalishaji kiwanda cha Bakhresa Buguruni, Profesa Mkumbo alisema ameambiwa ipo fursa kubwa kwa wakulima wa ngano ambao wanatakiwa kuichangamkia.

“Wakulima wa zao la ngano wanatakiwa kujiunga katika ushirika na siyo kufanya kilimo cha mtu mmoja mmoja, mahitaji ya malighafi ya viwandani hivi yanatoka nje hivyo ipo fursa hapa kwa wakulima wa ndani," alisema.

Profesa Mkumbo aliahidi kuzungumza na Wizara ya Kilimo ili kuona umuhimu wa wakulima kuwekeza katika eneo hilo.

Alisema hawawezi kutosheleza eneo hilo kwa mkulima mmoja mmoja hivyo, lazima wajiunge ili wakopesheke na taasisi za fedha na kuzalisha mazao bora yanayokubalika ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Kampuni ya Bakhresa Group, Hussein Sufian alisema serikali imeonesha nia ya dhati ya kuwekeza katika viwanda na wanaamini yaliyojadiliwa siku hiyo yatasaidia kukuza uwekezaji uliopo na unaokuja.

Sufian alisema Bakhresa ana jumla ya kampuni 17 zinazozalisha bidhaa mbalimbali zinazouzwa ndani na nje ya nchi na kutaja baadhi kuwa ni Kenya, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, China na Yemen.

Pia alisema anashukuru kwa sasa yapo mabadiliko makubwa, wanapata ushirikiano mkubwa kutoka taasisi za uthibiti na uwekezaji na misuguano iliyokuwepo awali imepungua.

Awali akiwa kiwanda cha Knauf kilichopo Mkuranga, Profesa Mkumbo aliwapongeza kwa uwekezaji huo ambao unazalisha ajira kwa wazawa na kutunza na kuheshimu utu wa Watanzania.

Chanzo: habarileo.co.tz