Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkulima ataka mbolea ifungwe uzito wa kilo tano

Mbolea Mkulima ataka mbolea ifungwe uzito wa kilo tano

Wed, 1 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amelipokea ombi la mkazi mmoja wa Kijiji cha Ulemo kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani Singida aliyetaka mbolea ya ruzuku wanayouziwa ifungwe katika uzito tofauti ili mkulima anunue kiwango anachotaka.

Hoja hiyo imeibuliwa leo Machi Mosi, 2023 wakati wa mkutano wa wanachama wa CCM katika shina namba 6 ambapo Chongolo amepokewa na kushiriki mkutano huo wa chama ngazi ya shina.

Moja ya changamoto zilizoibuliwa na mjumbe wa mkutano huo, Mark Makala ni baadhi ya wakulima kushindwa kumudu bei ya mbolea kulingana na ujazo wa kilo 50 zinazouzwa, hivyo ametoa ombi la kutaka mbolea hizo zipakiwe kwenye ujazo wa kilo tano ili kila mkulima amudu bei hizo.

"Tunaipongeza serikali kwa kutupatia mbolea ya ruzuku, lakini tunaomba ikiwezekana mbolea ipakiwe kwenye kilo tano ili kila mwananchi aweze kununua. Wengi tunashindwa kununua hii ya kilo 50, lakini ikiwepo ya kilo tano, kila mtu ataweza kununua," amesema kada huyo wa CCM.

Akizungumzia changamoto hiyo, Chongolo amesema amelipokea na analibeba kwa ajili ya kushinikiza utekelezaji wake.

"Suala la vifungashio, hilo nimelibeba. Ni kweli linatakiwa kuangaliwa kwa namna tofauti. "Kama sukari tuna kilo tano, kilo mbili na kilo moja, mbolea inashindikana nini? Tuweke vipimo ili kila mtu anunue kiwango anachotaka, pengine mtu mahitaji yake ni kilo 10 tu, au tano," amesema Chongolo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live