Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkonge kuokoa bil 580/- za vifungashio

Be5388f4c67709c0069f08fa588b8ecf.png Mkonge kuokoa bil 580/- za vifungashio

Thu, 21 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, jana aligawa miche ya mkonge na kueleza namna zao hilo linavyoweza kumtajirisha mkulima kwa kupata mavuno makubwa na fedha nyingi hata akilima kwenye eneo dogo.

Alisema, kulima mkonge kuna faida kubwa na kwamba mkulima anaweza kuvuna tani moja kwenye hekta moja (ekari mbili na nusu) hivyo kupata faida ya zaidi ya sh milioni tatu baada ya kutoa gharama za uzalishaji.

Aliyasema hayo jana mkoani Tanga wakati akizungumza na wadau wa mkonge akiwa kwenye ziara kuhamasisha kilimo cha zao hilo. Majaliwa alisema ili kuandaa eneo hilo mkulima anaweza kugharamia Sh 50,000/- za kukodi trekta la kusafisha eneo, atahitaji miche 1,600, na kwamba, kila mche ataununua kwa bei ya wastani ya Sh 200/-.

Alisema mkulima huyo hadi kipindi cha mavuno atakuwa ametoa takribani Sh 560,000/- zikiwemo gharama za vibarua wa kupanda, wa kupalilia na fedha za dharura zikiwemo za dawa.

“Kama makuzi yamekwenda vizuri kwenye hekta moja unaweza kuvuna tani moja, kiwango cha chini lakini unaweza kuvuna tani moja na nusu na kuendelea. Kwa kilimo hiki cha kawaida, hapo hujaweka utaalamu” alisema Majaliwa.

Alisema tani moja ya daraja la juu la mkogwe inauzwa sh milioni nne, daraja la chini sh 3,500,000/-, hivyo ukiondoa gharama za tangu kuandaa shamba hadi kuvuna kinachobaki ni faida.

Alisema mkonge unalimwa kwenye mikoa zaidi ya mitano kwa sasa na kwamba serikali imeamua kupeleka uchumi kwa mtu mmoja mmoja, kutengengeza fursa za ajira, na kuongeza viwanda ili kuboresha maisha ya wananchi “Tumeamua kuliwekea nguvu zote ili tulilime, lilikuwepo, lilikufa.

Tumeamua kulifufua na jitihada za kufufua zao hili pia taifa litaokoa fedha Dola za Kimarekani zaidi ya dola 245 mpaka 250 (milioni) zinazotumika kuagiza vifungashio vinavyotokana na zao hili kutoka nje ya nchi”alisema Majaliwa.

Alisema wakulima wenye nia ya kulima mkonge wapo, uwezo wa kulima upo kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha na kwamba serikali imedhamiria kulifufua zao hilo.

“Haya lazima tuwaambie wakulima wetu kwamba kulima mkonge leo ni faida tupu. Na haya tunayasema wenye nia njema, wasiokuwa na nia njema hawatoyasema.”alisema

Majaliwa na kubainisha kuwa ukilima mkonge utakuwa unavuna kwa miaka 15. Alisema sanjari na mkonge pia serikali imeongeza zao la chikichi kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati.

Alisema, kilimo cha chikichi kinaiwezesha serikali kuokoa Dola za Marekani milioni 470 kwa mwaka ambazo zingetumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Juni mwaka jana Majaliwa alifanya ziara Tanga maalumu kwa ajili ya mkonge na akabainisha kuwa zao hilo lina faida nyingi na ndio maana bei yake iko juu.

“Serikali inamshukuru sana Mkuu wa Mkoa wenu wa Tanga ambaye alianza kufuatilia mkonge akagundua kwamba bei ya mkonge tani moja ni zaidi ya shilingi 3,600,000/- lakini mkulima wa Tanga alikuwa hapati hizo milioni 3,600,000/- anaishia kwenye laki moja, laki mbili au zinaishia zote kwenye makato. Sasa tutahakikisha mnapata fedha hiyo”alisema Majaliwa.

Alisema mkonge si kwa ajili ya nyuzi tu, unatumika pia kutengenezea pombe, gesi, mbolea, dawa za binadamu na mifugo. Aliagiza Serikali iwape msaada watu wanaotaka kulima mkonge kwenye mkoa wowote wenye ardhi inayofaa kwa zao hilo bila kujali kama ni mkulima mkubwa, wa kati au mdogo, na kwamba wakulima watafutwe, wajitambulishe, na wasaidiwe.

“Na ukipata mwekezaji kutoka popote, walioko ndani leo na wanaokuja wote hao wapokelewe, wasaidiwe, waendeshe biashara yao ya kilimo cha mkonge. Ninaambiwa hapa kuna baadhi ya wawakilishi wa wakulima, limeni mkonge”alisema Majaliwa.

Jana asubuhi Majaliwa aligawa miche ya mkonge na kuziagiza Halmashauri zinazolima zao hilo zitenge eneo lisilopungua ekari 10 kwa ajili ya kuandaa miche ili iwepo ya kutosha. Aidha aliziagiza taasisi na wajasiriamali zinazowekeza kilimo cha mkonge ambazo zinamiliki mashamba makubwa ziandae kitalu cha mbegu za mkonge kwa ajili ya wananchi ili kuondoa upungufu.

Majaliwa alitoa agizo hilo akiwa kwenye Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kituo cha Mlingano wilayani Muheza mkoani Tanga. Alikwenda huko kugawa miche na kujionea hali halisi ya zao hilo baada ya kutoa maelekezo ya kuzalisha miche ya mkonge kwa wingi Juni mwaka jana.

“Utekelezaji wa agizo hili na uanze sasa ili kuanzia mwaka ujao miche hiyo ianze kukabidhiwa kwa wananchi,” alisema na kuongeza; “Kituo chetu cha Mlingano licha ya kuendelea na uzalishaji wa miche kiendelee na kujikita katika utafiti wa mbegu bora pamoja na dawa za kudhibiti magonjwa katika zao hilo lakini uzalishaji liwe suala la wote”.

Majaliwa pia aliiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) iweke masharti kwa wawekezaji wenye mashamba makubwa kuwa ni lazima wawe na vitalu vya miche kwa ajili ya kugawa kwa wakulima wadogo wanaozunguka maeneo yao.

Majaliwa alisema lengo la serikali ni kuhakikisha mpaka ifikapo mwakani kuwe na ongezeko la uzalishaji wa miche zaidi ya milioni mbili ya sasa kwani mahitaji ni makubwa.

Mkurugenzi wa TARI Mlingano, Dk Catherine Senkoro, alisema kituo hicho kimeongeza uzalishaji wa miche bora ya mkonge aina ya chotara 11,648 ambapo kufikia Oktoba 2020, eneo lenye ukubwa wa hekta 65 sawa na eka 162.5 limetolewa visiki na kusafishwa. Alisema hekta 31.2 sawa na eka 78 ambayo ni sawa na asilimi 48 ya eneo lote lililosafishwa limepandwa miche ya mkonge milioni 2.5.

“Mpaka kufikia Januari, 2021 jumla ya hekta 32.6 sawa na eka 81.5 zimepandwa miche ya mkonge katika maeneo ya TARI Mlingano, Halmashauri ya Muheza hekta moja na Gairo hekta 0.4. Pamoja na miche iliyokuwa shambani kabla ya Juni 2020, jumla kuu ni miche 2,672, 000,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TARI, Dk Yohana Budeba alisema bodi ilitoa maagizo kituo hicho kizalishe mbegu bora na za kutosha ili wakulima walime kilimo cha kisasa.

Dk Budeba alisema kituo hicho mbali na kuzalisha mbegu bora kinatoa mafunzo kwa wananchi lakini pia ni shamba darasa la kusaidia wananchi. Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo alisema zao la mkonge ni miongoni mwa mazao saba ya kimkakati ambayo serikali imeweka nguvu ili kuchangia uchumi wa taifa.

Dk Mkamilo alisema zao hilo linalimwa mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Tanga, Pwani, Lindi, Morogoro, Kilimanjaro, Shinyanga, Arusha, Simiyu na Mara. Alisema hapa nchini utafiti unaonyesha kuwa hekta 44,000,000 zinafaa kwa ajili ya mkonge, mpaka sasa asilimia 0.2 ndizo zilizolimwa mkonge nchini.

“Kwa kuliona hilo Waziri Mkuu ameweka msukumo mkubwa kwenye hili zao ili nchi izalishe kwa wingi,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema serikali ilitoa sh. milioni 700 kwa ajili ya shughuli za kilimo ambapo kiasi cha fedha hizo kilitumika katika kuanza uzalishaji wa mbegu za mkonge. Alisema changamoto ya upatikanaji wa mbegu itaweza kumalizika kama serikali itaweza kuwaboreshea maabara ya uzalishaji wa chupa kituo cha TARI Mlingano ili kuongeza kasi ya uzalishaji.

“Tunaiomba serikali kutuboreshea maabara hapa Mlingano ili badala ya kuendelea na uzalishaji wa kienyeji sasa tuhamie kwenye maabara ambapo tutakuwa na uhakika wa mazao bora ambayo hayataweza kupambana na magonjwa” alisema.

Alisema iwapo kutakuwa na uhakika wa maabara bora hata Halimashauri zikianzisha vitalu itaweza kuzalisha mbegu nyinyi ambazo zitagawiwa kwa wananchi. Imeandikwa na Lucy Ngowi na Amina Omari, Muheza.

Chanzo: habarileo.co.tz