Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkataba wa ukarabati mabehewa wasainiwa

Thu, 14 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wametiliana saini mkataba wa ukarabati wa mabehewa 40 ya mizigo ili kuongeza kiwango cha usafirishaji mizigo kwa TRC.

WFP imetoa Sh1.3 bilioni (Dola 600,000) kwa ajili ya ukarabati huo na kama mdau wa usafirishaji, WFP itapata fursa ya kusafirisha mzigo mwingi zaidi kutoka sehemu mbalimbali kwenda maeneo yenye uhitaji wa chakula nchini na nchi za jirani kama Uganda na Sudan Kusini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo leo Jumatano Machi 13, 2019 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe amesema makubaliano hayo yataiongezea uwezo TRC wa kusafirisha mizigo kwenda nchi jirani.

“Nchi za jirani wana mizigo mingi wanataka kuisafirisha lakini uwezo wa reli yetu ni mdogo. Reli hii ya kati ina uwezo wa kusafirisha tani milioni tano za mzigo, lakini hatufikii kiwango hicho. Uganda wana mizigo mingi, DRC wana mizigo, Rwanda na Burundi wana mizigo, hizi ndiyo fursa tunazotakiwa kuzifikia,” amesema Kamwelwe.

Amesema Serikali ilitoa Sh5 bilioni kwa ajili ya kukarabati mabehewa 200, mpaka sasa tayari mabehewa 40 yamefanyiwa ukarabati huo. Amesema miradi hiyo miwili ikikamilika, jumla ya mabehewa 240 yatakuwa yamekarabatiwa.

Waziri huyo amesema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya usafiri wa reli ili ifanye kazi ya kufikia malengo ya Serikali. Amesisitiza kwamba tayari kilomita zaidi ya 900 zimekarabatiwa katika Reli ya Kati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TRA, Masanja Kadogosa amesema shirika hilo linatekeleza mradi wa ukarabati wa mabehewa ya abiria na mizigo na kwamba kuna mabehewa zaidi ya 1,000 ambayo yanahitaji kukarabatiwa.

Amesema mradi huo unatarajiwa kutoa ajira za kudumu 30 na ajira nyingine za muda mfupi kwa watu 32 watakaofanya kazi ya ukarabati huo. Amesema mradi huo ukikamilika utaliwezesha shirika hilo kusafirisha mizigo mingi kwa wakati mmoja.

“Sasa tumewekeza nguvu kubwa ya kufungua njia kutoka Tanga kwenda Arusha. Tunashukuru pia WFP wametusaidia katika kurudisha njia ya reli inayokwenda Uganda,” amesema mkurugenzi huyo.

Mwakilishi mkazi wa WFP, Michael Dunford amesema shirika lake linakusudia kununua tani 120,000 mpaka 160,000 za chakula hapa nchini na kuzipeleka katika maeneo mbalimbali yenye uhitaji ikiwemo Uganda na Sudan Kusini.

“Itakuwa haina maana kama tutanunua mzigo mkubwa halafu tukashindwa kuusafirisha kwenda sehemu inayohitajika. Ndiyo maana tumeona ni vema tukashirikiana na TRC katika kukarabati mabehewa ili yaweze kuhimili wingi wa mizigo,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz