Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkataba wa mafuta, gesi Bara na Z’bar wasainiwa

Ffc2349611f5d469136cd5c1348f9b0b Mkataba wa mafuta, gesi Bara na Z’bar wasainiwa

Sun, 20 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hati za makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi asilia kwa taasisi zinazoshughulikia sekta hiyo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar zimesainiwa na hivyo kufanya ushirikiano huo kuwa rasmi.

Hafla ya utiaji saini hati hizo ilifanyika jana Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.

Baadhi ya viongozi hao ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Dk Mngereza Miraji Mzee, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Magharibi, Rashid Msaraka na Meya wa Zanzibar, Mahmoud Mussa.

Wengine ni wakuu wa taasisi zinazosimamia sekta ya mafuta na gesi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wenyeviti wa bodi za taasisi hizo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Zanzibar, Dk Mngereza Miraji Mzee alisema taasisi zilizosaini makubaliano hayo ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC).

Nyingine ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura) na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura).

Alisema TPDC na ZPDC zitashirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwamo kujenga uwezo kwa wataalamu pamoja na kubadilishana wataalamu, vifaa na teknolojia katika masuala yanayohusu utafutaji mafuta na gesi asilia katika pande mbili za muungano.

Aidha, ushirikiano huo utafanywa katika eneo la kubadilishana uzoefu kwenye kuchakata, kutafsiri na kutunza takwimu na taarifa mbalimbali zinazohusu utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia.

Kuhusu Pura na ZPRA, ushirikiano utakuwa kwenye kubadilishana uzoefu katika kuandaa na kutunga miongozo na kanuni mbalimbali zitakazosimamia shughuli za mkondo wa juu wa petroli.

Pia kuongeza ujuzi katika kufanya kaguzi za mikataba ya ugawanaji mapato, kubadilishana uzoefu katika kusimamia utunzaji wa taarifa za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia na kushirikiana kwenye eneo la mkondo wa juu wa petroli.

Aidha, alisema Ewura na Zura zitashirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwamo kutoa ushauri wa kitaalamu wakati wa kutayarisha nyenzo za kiudhibiti, kubadilishana uzoefu wa kiudhibiti katika maeneo ya kiufundi na kiuchumi katika sekta za nishati na maji ikiwamo ukokotoaji wa bei, gharama za huduma na mambo mengine.

Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Msaraka ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi alisema utiaji saini wa makubaliano hayo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi wakuu wa pande zote mbili za muungano pamoja na mawaziri wanaosimamia sekta hizo ambao wameonyesha umakini katika kusimamia sekta hizo.

Alisema taasisi hizo zilikuwa zikishirikiana ila sasa imekuwa rasmi na utendaji wenye tija utaonekana zaidi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba alisema tukio hilo lengo lake ni kuboresha na kuimarisha shughuli za utafiti wa mafuta na gesi.

Alisema hadi sasa kiasi cha gesi kilichogundulika ni futi za ujazo zaidi ya trilioni 57 na bado kuna dalili za upatikanaji mafuta.

Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Dk Hussein Mwinyi alisema Zanzibar inakusudia kuchimba mafuta na gesi kuanzia mwaka huu baada ya kubainika kuwapo kwa hazina ya rasilimali hiyo inayofikia futi za ujazo trilioni 3.8.

Katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Ikulu Zanzibar, Dk Mwinyi alisema uamuzi huo umekuja baada ya majibu ya matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni iliyopewa kazi hiyo ya Rakgas kutoka Falme za Rasilkhema kuonesha kipo kiwango kikubwa cha hazina ya mafuta na gesi.

Alisema utafiti huo umefanywa katika maeneo ya ardhini na baharini hadi angani na kuonesha yapo matumaini makubwa ya hazina ya mafuta na gesi.

“Nataka niwajulishe wananchi matokeo ya utafiti uliofanywa wa mafuta na gesi unaonesha kipo kiwango kikubwa cha hazina ya mafuta na gesi katika visima vyote vilivyopo Unguja na Pemba,” alisema Dk Mwinyi.

Aidha, aliwahakikishia wananchi kwamba mafuta na gesi itakayochimbwa itawanufaisha wananchi moja kwa moja pamoja na kuwapo kwa mikataba yenye maslahi na taifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live