Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) umeanza kuleta matokeo chanya baada ya mfanyabiashara wa kwanza, Shabani Hamis kupatiwa cheti maalumu cha uasilia wa bidhaa zinazotoka Tanzania.
Akikabidhi cheti hicho jana Jumanne, Mei 9, 2023 jijini Dar es Salaam, Kaimu Makamu wa Rais upande wa Viwanda wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Vicent Minja alisema kupitia cheti hicho mfanyabiashara huyo atapata punguzo la Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 35 hadi 12.
"Kutokana na uhamasishaji wetu sisi TCCIA kwa kuwaelimisha wafanyabiashara manufaa ya kusafirisha bidhaa hapa barani ukiwa na cheti cha uasilia wa bidhaa chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika jana tumemkabidhi mfanyabiashara wa kwanza cheti cha uasilia ikiwa ni matunda ya mkataba huu," alisema Minja.
Minja aliwataka wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa zinazopatika ndani ya soko huru la Afrika kwa kufika katika Chemba ya biashara ambayo ndio ina jukumu la kutoa vyeti hivyo ikiwa ni pamoja na kupatiwa elimu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (Tantrade), Fortunatus Mhambe alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifanya biashara lakini hawaoni umuhimu wa kupata cheti cha uasilia ambacho humsaidia mfanyabiashara mwenyewe.
"Afrika imekuwa ikipambana na changamoto nyingi za kiuchumi lakini sasa kuna hii fursa kubwa ambayo sisi Watanzania lazima tuichangamkie," alisema Mhambe.
Mhambe alisema soko huru la biashara ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara nchini kwani hata mkataba huo wa biashara huru unazingatia kupunguza vikwazo vya kibiashara kila siku huku akiwahamasisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo.
Naye mfanyabiashara Shabani Hamis alisema anaishukuru TCCIA kwa kuleta Mkataba wa uasilia wa bidhaa kwa sababu cheti alichokabidhiwa kitasaidia kuwaongezea wateja zaidi hasa nchini Algeria ambako ndiko huuza zao la kahawa kwa kupunguza asilimia kubwa ya ushuru.
"Napenda kuwashukuru TCCIA kwa fursa hii waliyotutengenezea ya kututanulia soko na wateja kuongezeka. Nina imani mpaka mwakani tutaweza kusafirisha mpaka tani 1000 za Kahawa nje ya nchi," alisema Hamis.
Hamis alisema anapeleka kontena 9 za Kahawa (Green Robuster) nchini Algeria ambazo ni sawa na tani 172.8 ambapo tayari kontena hizo zilishaondoka nchini tangu Aprili 29, 2023 na sasa anakamilisha suala la cheti cha uasilia.
"Tuna mazao mengine kama Kokoa na Korosho ambapo tunatazamia kutumia fursa hii kuongeza wateja katika bidhaa zetu nyingine," alisema Hamis.
Aidha aliishukuru Serikali kupitia wizara ya Viwanda na Biashara na Tantrade kwa kuweka mazingira wezeshi kibiashara ikiwemo kuondoa vikwazo vya kibiashara Afrika jambo lililowapa uhuru wa kufanya biashara barani.