Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkapa atoa mbinu za kufikia uchumi wa kati

10949 MKAPA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bariadi/Morogoro. Rais mstaafu Benjamin Mkapa ametoa mbinu kwa wananchi ya kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.

Ameishauri Serikali na wadau wengine kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha malighafi inapatikana kwa viwanda vinavyoendelea kujengwa.

Mkapa alisema hayo jana alipomwakilisha Rais John Magufuli katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

Akitumia salamu yake maarufu ya ‘mambo’ na kuitikiwa na wananchi waliohudhuria maonyesho hayo ‘poa’, Mkapa aliwataka Watanzania kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 65 ya watu nchini.

Alisema kwa kufanya hivyo pia watawezesha kutekelezwa kwa sera ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Mkapa alipongeza juhudi za kuongeza matumizi ya pembejeo ikiwamo mbolea, akisisitiza uamuzi wa Serikali wa kuondoa zuio la kuuza mazao nje ya nchi ili kutoa fursa ya soko na mapato kwa wakulima.

“Hata hivyo, wanaotaka kuuza mazao nje ya nchi watalazimika kufuata sheria, kanuni na utaratibu. Pia lazima kila mmoja na sote kwa pamoja kama Taifa tuhakikishe tunaweka na kutunza akiba ya kutosha ya chakula kulingana na mahitaji ya Taifa,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya wadau wengine wa maendeleo ya sekta ya kilimo, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (Fao), Fred Kafeero alisema wataendelea kushirikiana na Serikali kuwekeza juhudi, nguvu, maarifa na mitaji kuboresha sekta ya kilimo.

“Uhakika wa chakula na lishe bora kwa kila nchi ndiyo kipaumbele cha kwanza cha Fao; tutaendelea kushirikiana na kuhakikisha Tanzania inazalisha chakula cha kutosheleza mahitaji,” alisema Kafeero.

Akizungumza katika sherehe hizo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mara inaburuta mkia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ilani ya uchaguzi ya CCM.

Tofauti na mikoa hiyo, alisema Simiyu ndiyo kinara katika utekelezaji wa ilani hiyo na miradi ya maendeleo.

Alisema mikoa mingine inayofanya vyema katika utekelezaji wa miradi na ilani ya CCM ni Singida, Dodoma na Pwani.

Dk Bashiru alitaja siri ya mafanikio ya Simiyu kuwa ni ushirikiano, mshikamano na kuzungumza lugha moja kati ya viongozi wa Serikali na wa CCM.

“Viongozi katika mikoa niliyoitaja kufanya vibaya hawapikiki chungu kimoja; mahusiano yao ni kama ya paka na panya. Mkoa wa Mara ndiyo kinara wa migogoro kati ya viongozi wa chama na Serikali ukifuata Arusha, Mbeya na Dar es Salaam.

“Naamini katika misingi mitatu ya mshikamano, nidhamu ya utendaji na nguvu ya kujitegemea kama njia ya kufikia mafanikio ambayo kila kiongozi anayataka.”

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alitaja siri ya mafanikio katika mkoa wake kuwa ni makubaliano miongoni mwa viongozi ya kila mmoja kuchapa kazi na kutimiza wajibu wake pale alipo.

“Nakuhakikishia (Dk Bashiru) kuwa umoja, mshikamano na ushirikiano Simiyu hauko miongoni mwetu viongozi wa mkoa pekee; uko vivyo hivyo ngazi ya wilaya, kata, vijiji hadi vitongoji,” alisema Mtaka.

Alisema pia wameweka mipaka ya kiutendaji kati ya wanasiasa na watumishi wa umma.

“Viongozi wa Serikali mkoani Simiyu wako kwa ajili ya kuchapa kazi na si kuingilia wala kuandaa safu za uongozi ndani ya chama. Hii imewafanya viongozi wa kisiasa kujiamini na kushirikiana na wale wa Serikali kuchapa kazi kwa bidii kutekeleza miradi ya maendeleo na ilani ya CCM,” alisema Mtaka.

Nanenane kwingineko

Katika maadhimisho hayo mkoani Morogoro, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhanga Mpina alikemea kamatakamata ya mifugo iliyokithiri maeneo mengi nchini, akiwataka viongozi wanaofanya hivyo kuacha mara moja.

Akizungumza katika maonyesho ya wakulima Kanda ya Mashariki inayohusisha mikoa ya Morogoro, Tanga, Pwani na Dar es Salaam, Mpina alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali kujichukulia hatua na kufanya operesheni ya kukamata mifugo bila kufuata sheria na utaratibu.

“Viongozi lazima tufuate sheria ili kuondoa migogoro, nasisitiza watendaji wote wafuate utaratibu,” alisema.

Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji alisema imepungua, hivyo aliagiza wakuu wa wilaya na mikoa kuimaliza.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama akizungumza mkoani Arusha aliwataka wakuu wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini kuhakikisha wanatatua migogoro ya ardhi ya wakulima na wafugaji ili waondokane na tatizo hilo.

Peter Saramba (Bariadi), Lilian Lucas (Morogoro) na Joseph Lyimo (Arusha)

Chanzo: mwananchi.co.tz