Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkandarasi ujenzi kiwanja cha ndege Msalato apewa angalizo

14405b2c003c212a2afbb06968ae84da Mkandarasi ujenzi kiwanja cha ndege Msalato apewa angalizo

Wed, 17 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amemtaka mkandarasi anayejenga Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato mkoani Dodoma kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa kiwanja hicho kwa wakati na kwa ubora.

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wenye urefu wa kilometa 3.6 unatarajiwa kukamilika Juni, 2025 na utagharimu takribani Sh bilioni 165.

Profesa Mbarawa alitoa agizo hilo jijini Dodoma alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho.

Ujenzi wa uwanja huo unatekelezwa na Kampuni ya Sinohydro Corporation kwa kushirikiana na M/s Beijing Sino– Aero Construction Engineering na M/s China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation.

"Niwasisitize wale waliopata fursa ya kusimamia ujenzi wa kiwanja cha ndege hiki akiwemo Mhandisi Mshauri, Tanroads na TAA lazima tuhakikishe mkandarasi anajenga kwa viwango vinavyotakiwa na ikiwezekana hadi kufikia Juni 2025 mradi uwe umekamilika," alisema.

Profesa Mbarawa aliahidi kwamba atakuwa anautembelea mradi huo mara kwa mara ili kuona hatua mbalimbali za utekelezaji wake kuanzia mwanzo hadi mwishoni.

Lengo la kutembelea alisema ni kuona kama mkandarasi anafanya kazi kulingana na yale waliyokubaliana kwenye mkataba.

Aidha, Profesa Mbarawa alifafanua kuwa kiwanja hicho kinajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, Apron, Tax way na kufunga taa.

Katika awamu ya pili ujenzi wake ni wa jengo la abiria na miundombinu mingine inayotakiwa katika kukamilisha uwanja huo wa kimataifa.

Mbarawa alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini ili kuleta maendeleo kwa taifa kwa ujumla.

Aliwataka wananchi kuwapa ushirikiano wakandarasi hao ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unaisha kwa haraka na kuweza kuleta tija kwa jamii na taifa.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Dodoma, Leonard Chimagu, alisema kwa sasa mkandarasi anaendelea na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege.

Naye mkazi wa Msalato, Juma Aheri, alisema wanatarajia kupata ajira nyingi katika mradi huo. Pia akasema mradi ukikamilika eneo hilo litaendelea kiuchumi kwani biashara pamoja na hoteli zitajengwa kwa wingi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live