Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkakati wa kuitangaza Tanga kiutalii waanikwa

TANGA Mkakati wa kuitangaza Tanga kiutalii waanikwa

Thu, 30 Apr 2020 Chanzo: --

WIZARA ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Halmashauri za Mkoa wa Tanga, inapitia vivutio vya utalii vilivyoko mkoani huko ili kuviendeleza na kuvitangaza.

Vilevile, imeelezwa kuwa Sekta ya Utalii kwa mwaka 2019, ilichangia takriban Dola za Marekani bilioni 2.6 katika uchumi wa nchi.

Hayo yalibainishwa na wizara hiyo jana bungeni jijini hapa ilipojibu swali la Mbunge wa Kilindi (CCM), Omari Kigua.

Katika swali lake, mbunge huyo alisema Sekta ya Utalii ni moja kati ya vyanzo vikuu vya mapato kwa uchumi wa nchi na serikali ina dhamira ya dhati kuinua sekta hiyo.

“Kilindi ni moja kati ya maeneo yenye vivutio vya utalii kama vile mlima mfano wa mama aliyembeba mwana, Pori Tengefu la Handeni pamoja na maeneo yenye uoto wa asili katika Kata ya Lwanda Kijiji cha Lukigo,” alisema.

Mbunge hyo alihoji mpango wa serikali kuyatambua rasmi maeneo hayo ya utalii.

Katika majibu yake kwa mbunge huyo, wizara hiyo ilisema inafanya mapitio kwenye mkoa huo kwa kuviangalia vivutio vilivyoko wilayani Kilindi, likiwamo Pori Tengefu la Handeni.

Ilisema ina jukumu la kubaini, kuendeleza na kutangaza vivutio vya utalii nchini kwa kushirikiana na mamlaka za halmashauri za miji, manispaa na wilaya.

“Katika kutekeleza jukumu hilo, wizara inaendelea kubaini vivutio vya utalii katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuhamasisha uendelezaji wake na kuvitangaza ili maeneo hayo yatembelewe na watalii na kuongeza kipato,” ilisema.

Wizara hiyo ilisema kuwa katika Mkoa wa Tanga, kazi hiyo imeshafanyika kwenye Wilaya za Tanga Mjini, Muheza, Pangani na Mkinga na kazi hiyo ni endelevu.

Ilisema sekta ya utalii huchangia zaidi ya asilimia 25 ya mauzo yote ya nje na hutoa ajira zaidi ya milioni 1.5 kati ya ajira zote za moja kwa moja na zile ambazo si za moja kwa moja.

“Utalii ni sekta mtambuko, hivyo imeendelea kuwa chachu kwa maendeleo ya sekta nyingine za uchumi kama vile, kilimo, viwanda, huduma za fedha na miundombinu,” ilisema.

Chanzo: --