itaifa Mkakati kuwawezesha wanawake, wasichana kidigitali waja Ijumaa, Mei 12, 2023 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Selestine Kakele akizungumza leo Mei 12, 2023 katika Maktaba ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam New Content Item (1) By Emmanuel Msabaha Mwandishi wa habari Mwananchi Muktasari: Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imejipanga kuweka mikakati thabiti ambayo itawasaidia wanawake, wasichana kujikwamua kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali za kidigitali. Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema itahakikisha inaweka mipango thabiti ambayo itawasaidia wanawake, wasichana kujikwamua kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali za kidigitali.
Akizungumza jana Mei 12, katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele amesema ni muhimu kwa jinsia ya kike kupata fursa sawa ya kustawi katika uwezo wa kidigitali kama ilivyo kwa jinsia ya kiume. “Elimu ya kidigitali si anasa ni jambo la lazima katika ulimwengu huu wa sasa, hivyo tutahakikisha wanawake na wasichana wanapata elimu zaidi kuhusu suala hili,” amesema.
Kakele ambaye alimuwakilisha Naibu Waziri wa Wizara hiyo ameeleza kwamba, kama wizara husika watahakikisha wanashughulikia pengo linalozidi kukua kati ya wanawake na wanaume katika masuala ya kidigitali, hivyo kwa kupitia jukwaa la Panda Digital watashirikiana nao bega kwa bega. “Lazima tutengeneze mazingira wezeshi kwa wanawake, wasichana kwa kukuza na kuendeleza biashara zao kwa mfumo wa Kidigitali” amesema Pia amesema, wizara itahakikisha wanapitia sheria na sera zilizowekwa ili kuhakikisha kuna usawa kati ya wanawake na wanaume. Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Her Initiative, Lydia Moyo amesema kuhusu jukwaa la Panda Digital lengo lao ni kuhakikisha wanawasaidia wasichana, wanawake kupata ujuzi na rasilimali za kuanza na kuendesha biashara zao ili kufikia uchumi wa kidigitali. “Zaidi ya wasichana 2,265 wamenufaika na Panda Digitali kwa kufikia malengo yao katika biashara za teknolojia” amesema. Ameongeza na kusema pamoja na mambo yote hayo bado kuna changamoto ya elimu ya Kidigitali kwa upande wa wanawake hivyo watahakikisha wanatoa ujuzi na elimu kwa jinsia hiyo. “Nina amini wizara husika itahakikisha inafuatilia changamoto zote na kuzitolea ufumbuzi ikiwemo kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa kesi za mtandaoni kuhusu masuala ya unyanyasaji” amesema Naye, Lilian Mwamdanga kwa niaba ya Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa wanawake nchini amesema UN itahakikisha inasimamia suala la usawa wa jinsia kati ya wanaume na wanawake katika biashara za kidigitali. “Tunatakiwa kuchukua hatua thabiti ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za biashara mbalimbali za kidigitali kama ilivyo kwa jinsia ya kiume” amesema. Diana Mshana ambaye ni mmoja katika ya vijana waliohudhuria hafla hiyo, amesema changamoto ambazo wanakumbana nazo ni watu kutokuwa na elimu ya kutumia mitandao ya kijamii, hivyo anaamini kupitia jukwaa la Panda Digital watajifunza vitu vingi ambavyo vitakuwa mwanga katika kuendeleza biashara zao.