Serikali ya Uholanzi na taasisi zinazoshughulikia masuala ya uwekezaji na biashara Tanzania,wamekutana na wawekezaji,wafanyabiashara kutoka nchi hizo kujadili changamoto katika biashara na uwekezaji hapa nchini na namna ya kuzitatua.
Akizungumza jijini Arusha katika mkutano wa kujadili masuala ya biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe De Boer,alisema majadiliano hayo ni muhimu baina ya nchi hizo na yatawezesha kufungua fursa za uwekezaji hapa nchini na kuimarisha uchumi wa Tanzania.
Alisema kupitia majadiliano hayo yatatumika kama jukwaa la kujadili juhudi za pamoja za kukuza mazingira bora ya biashara na uwekezaji ili iweze kuwa kivutio zaidi cha uwekezaji chenye ushindani.
Alisema wameridhishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja na kuondoa vikwazo mbalimbali katika sekta hiyo.
“Uhusiano baina ya Tanzania na Uholanzi ni mkubwa na unategemea zaidi ushirikiano endelevu wa biashara na tumekuwa mshirika mkubwa maendeleo wa Tanzania kwa muda mrefu na kampuni nyingi za Uholanzi zimefanya uwekezaji Tanzania,”alisema
Alisema kuwa lengo la mazungumzo hayo ni kujadili changamoto za kibiashara na uwekezaji kwa wawekezaji kutoka Uholanzi ambao wanawekeza hapa nchini na namna ya kuzitatua kwa kushirikiana kwani biashara imekuwa kichocheo cha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
“Mazungumzo haya ni muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji wa Uholanzi nchini Tanzania kwani ni muhimu kutambua mashirika ya kimataifa yamewekeza kwa kiasi kikubwa na mchango wake utaharakisha maendeleo hapa nchini,”aliongeza
Akifunga majadiliano hayo Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, alisema Uholanzi ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo.