Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mizigo ya DRC yaongezeka bandari ya DSM asilimia 15

Wabunge EALA Wahadharisha Ubaguzi Uwekezaji Wa Bandari Mizigo ya DRC yaongezeka bandari ya DSM asilimia 15

Tue, 26 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema mizigo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inayopitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam inazidi kuongezeka. Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dk George Fasha alisema hayo Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa ofisi ya biashara ya madini chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Madini Congo (CEEC).

Dk Fasha alisema DRC kufungua ofisi yake ya biashara ya madini nchini ni jambo muhimu kwa ustawi wa TPA kwani wamekuwa wakifanya nao biashara ya kupitisha mizigo inayoingia na inayotoka nchini humo.

“Tukichukulia namba toka mwaka 2018/2019, tukiangalia kipi kilitoka kipi kiliingia kwa DRC, tulipitisha tani milioni 1.9, lakini kwa mwaka tulioufunga 2022/2023 wenzetu wa DRC wametumia Bandari ya Dar es Salaam kwa kupitisha mizigo yenye thamani ya tani milioni 3.4 hili ni ongezeko kubwa sana,” alisema Dk Fasha.

Alisema TPA inachukulia soko la DRC ni lenye umuhimu mkubwa kwa sababu ya ongezeko la usafirishaji mizigo. “Tuna masoko kama sita, lakini la Congo ni muhimu sana…tukijaribu kufananisha robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 ilikuwa tani milioni 1.9 na robo ya kwanza ya 2023/24 tuna tani milioni 2.3 hiyo ni ongezeko la asilimia 15,” alifafanua Dk Fasha.

Aliongeza: “Tukifananisha Bandari ya Dar es Salaam na bandari shindani ambazo pia zinaweza kutuma na kupokea mizigo kutoka Congo, sisi tuna asilimia 68…kwa hiyo tukio hili kwetu ni muhimu sana kwa sababu linaenda kuimarisha mahusiano yetu ya kibiashara”.

Ofisi ya Ubalozi wa DRC nchini Tanzania imesema miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa na manufaa makubwa kwao. Ofisa ubalozi huo, Marcel Yampanya alisema ofisi hiyo itakayoshughulika na biashara ya madini ya DRC ni moja ya mafanikio ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

“Kumekuwa na mahusiano mazuri, sasa sisi tusaidie serikali zote mbili ziingize mapato ya kihalali kwenye biashara,” alisema Yampanya, katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Balozi wa DRC nchini, Jean Pierre Massala.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live