Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miundombinu bandari Ziwa Victoria yazidi kukamilika kusubiri shehena

Acb4a1d96ef820bb618d9a232eeaccf4 Miundombinu bandari Ziwa Victoria yazidi kukamilika kusubiri shehena

Wed, 7 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Daraja la reli, maalumu kwa kusafirisha mabehewa ni mojawapo ya miundombinu iliyo tayari katika bandari ya Kemondo, ikisubiri kuanza kwa safari za meli za mizigo.

Daraja hilo ni sehemu ya miundombinu iliyokarabatiwa hivi karibuni na mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Kiasi cha Sh milioni 800 kilitumika kwa ukarabati wa daraja hilo, jengo la abiria na vyoo katika bandari hiyo maalumu kwa mizgo mkoani Kagera.

Wadau wa maendeleo wameishauri serikali kuhimiza uwepo wa viwanda vya kutosha pamoja na uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kutosheleza mahitaji ya shehena kwa meli za mizigo zitakapokua zimeanza safari.

Walisema kiasi cha mizigo kinachopatikana kwa sasa bado kiko chini kwani hata meli ya abiria na mizigo iliyopo ya New MV Victoria Hapa Kazi tu, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mzigo haijawahi kufikisha hata nusu ya wastani wake wa mizigo.

“Sisi ni wafanyabiashara na watumiaji wa MV Victoria kwa muda mrefu tunafahamu. Ni wakati wa serikali kuweka mkazo wa uwekezaji ili meli za mizigo zifanye kazi kwa faida,” anasema mmoja wa wafanyabiashara na wasafirishaji wa mazao ya kilimo, hasa ndizi, Martin Kyomile.

Akizungumzia ushauri huo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Bukoba, Deodatus Kinawiro anasema kasi ya kuhimiza uwekezaji katika sekta za viwanda na kilimo ni kubwa, si tu kukidhi mahitaji ya meli za mizigo, bali pia kukuza uchumi wa watu binafsi na taifa.

Anasema wazalishaji wa juisi ya vanilla na maji safi ya kunywa, wazalishaji wa mabati na vyombo vya ndani vya plastiki pamoja na wa vinywaji vikali ni baadhi ya wawekezaji katika sekta ya viwanda ambao shughuli zao zitaanza hivi karibuni.

“Wameshatueleza uwezo wao wa kuzalisha na nia yao ya kusafirisha bidhaa zao kwenda maeneo mengine,” anasema Kinawiro.

Anaongeza kwamba sambamba na hilo, hivi karibuni lilifanyika tamasha la kibiashara katika wilaya yake na kukutanisha wawekezaji wa ndani na wa nchi jirani –Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan na DRC Congo.

Wawekezaji wa nje walionesha nia ya kuwekeza ila mchakato unazorota kutokana na mlipuko wa corona.

Pamoja na mlipuko huo mkuu huyo wa wilaya wa zamani anasema bado mawasiliano yanafanyika na uwekezaji utaanza mara moja baada ya hali kutulia, na kwamba tayari maeneo kadhaa yametengwa kulingana na mahitaji ya mwekezaji.

Kwa upande wa wawekezaji wa ndani, halmashauri imekua ikiwashirikisha wataalamu mbalimbali wa kilimo, wakiwemo watafiti ili kutoa elimu kwa wananchi ya kujikita zaidi katika kilimo cha biashara chenye tija na kukamata fursa mbalimbali za masoko katika mikoa mingine kwani tayari uhakika wa usafiri wa maji upo, na kwa gharama ya chini ikilinganishwa na njia zingine za usafirishaji.

Ushirikishwaji wa wataalamu wa kilimo tayari umezaa matunda ikiwa ni pamoja na kudhibiti ugonjwa wa ‘mnyauko’ uliokua ukiua migomba na hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa zao la ndizi.

Ni wataalamu haohao wamesaidia pia ongezeko la zao la kahawa kutoka tani 50,000 hadi 78,000 kwa msimu baada ya kutafiti na kusambaza mbegu bora, za kisasa na zinazotoa mazao haraka ikilinganishwa na zile za asili.

“Maboresho hayo katika sekta ya kilimo yamesababisha ongezeko la zao la ndizi ambalo ndilo husafirishwa kwa wingi na meli. Tafiti zinaendelea katika sekta ya kilimo na tutakua na mazao mengi ya kutosheleza mahitahi ya meli za mizigo. Tunapongeza bidii za mamlaka katika kuboresha bandari zetu,” anasema Kinawiro.

Baada ya Kemondo HabariLEO lilitembelea pia bandari ya Bukoba na kushuhudia maboresho ya miundombinu mbalimbali, ikiwemo jengo la abiria lenye uwezo wa kubeba watu 600 hadi 650 pamoja na maboresho ya eneo lenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 8,000 za mizigo kwa wakati mmoja.

Ofisi mbalimbali pamoja na vyoo ni sehemu pia ya miundombinu iliyoboreshwa katika mwaka wa fedha 2018/19 na kugharimu zaidi ya Sh 565 millioni.

Afisa Bandari, Denis Mapunda anaunga mkono hoja ya wadau wa maendeleo ya kuiomba serikali iongeze wigo wa uwekezaji katika sekta ya viwanda na kilimo ili kukidhi mahitaji ya meli za mizigo.

Anathibitisha kwamba meli ya MV Victoria haisafirishi zaidi ya tani 60 ikilinganishwa na uwezo wake wa tani 200.

“Tayari miundombinu yote iliyojengwa toka mwaka 1964 imeboreshwa. Upo mpango pia wa kupanua gati ili liwe na uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi, ikiwemo MV Mwanza inayojengwa kwa sasa mkoani Mwanza,” anasema.

Anasema maboresho yajayo, katika mwaka wa fedha 2021/22 yatahusisha pia ujezi wa miundombinu ya kuzuia nguvu ya mawimbi makali pamoja na upepo katika gati hiyo ambayo imechakaa.

Gazeti hili lilitembelea pia bandari ya Musoma mkoani Mara na kukuta maandalizi ya ukarabati wa daraja la reli yakifanyika.

Baadhi ya malighafi, hasa magogo tayari yalishakusanywa kama sehemu ya maandalizi ya ukarabati.

Hata hivyo, licha ya uwepo wa gati, bandari hiyo haifanyi kazi kwa sasa kutokana na kutokuwepo kwa meli yoyote.

Afisa Bandari, Almachius Vedasto, anashauri kwamba kwa matumizi bora ya bandari zilizoboreshwa na zinazondelea kuboreshwa na TPA, serikali iweke sheria ya kuwataka wasafirishaji wa shehena kubwa za mizigo kutumia usafiri wa maji.

Si tu kwa matumizi bora ya bandari bali hata kutunza miundombinu ya barabara kwani kusafirisha mizigo mikubwa kwa njia ya malori kumekua kukiharibu barabara.

“Kiwekwe kiwango cha mizigo kwa usafiri wa malori na mizigo mizito isafirishwe kwa meli,” anashauri.

Kutokana na ukosefu wa meli, kwa sasa wananchi wa Musoma wanategemea usafiri wa mashua kutoka mwalo wa Mwigobero, ambao uko jirani na bandari ya Musoma, kwenda visiwa mbalimbali vya Ziwa Victoria na maeneo mengie ya mkoa wa Mara, ikiwemo Wilaya ya Rorya.

Akizungumzia kuanza kwa matumizi ya madaraja ya reli katika bandari mbalimbali, Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni za huduma za meli (MSCL), Philemon Bagambilana anasema kwa kuanzia, bandari hizo zitahudumiwa na meli ya mizigo ya MV Umoja ambayo itafanyiwa ukarabati hivi karibuni.

Anasema baada ya ukarabati huo MV Umoja itaendelea na ratiba yake ya safari iliyozoeleka, ambayo ni kuhudumia bandari za ndani na nje, ikiwemo za Port Bell na Jinja (Uganda) pamoja na Kisumu (Kenya).

MV Umoja ilijengwa mwaka 1964 ikiwa na uwezo wa kubeba tani 1,200 au mabehewa 19 ya mizigo.

“Tuna miradi inayoendelea ya ujenzi na ukarabati wa meli. MV Umoja ni mojawapo,” anasema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz