Kutokana na uhaba wa maeneo ya kufanyia biashara ndogo Kariakoo, uongozi wa wafanyabiashara ndogo maarufu kama Machinga umetenga mitaa minne katika eneo hilo kwa ajili ya shughuli za wajasiriamali hao.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Taifa, Stephen Lusinde, alisema mitaa iliyotengwa ni Kongo, Nyamwezi, Swahili na Sikukuu, na alibainisha kuwa maeneo hayo yatatumika kipindi cha neema cha siku 12 zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla, kwa machinga kuhamia kwenye maeneo yaliyo rasmi.
Alisema hadi sasa wamefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 80 katika kutoa elimu juu ya suala la kuwapanga wafanyabiashara ndogo.
“Changamoto za hapa na pale zipo kwa sababu sisi ni binadamu, lakini ukizingatia mtu ana miezi sita au mwaka katika lile eneo kumhamishwa kidogo ni changamoto lakini tunaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa,” alisema Lusinde.
Pia alitolea ufafanuzi ugomvi uliojitokeza juzi katika eneo la Kariakoo wakati wakitimiza majukumu yao, akibainisha kuwa vurugu zilifanywa na vijana wahuni na sio wafanyabiashara.
Alisema vijana hao walikuwa na nia ovu ya kutaka kuharibu suala walilokuwa wakiliratibu.
“Kulikuwa kuna watu waliotaka kutumika, sisi hatuwezi kutafsiri sana kuwa ni kisiasa au ni kwa namna gani kuhakikisha wanaharibu hili zoezi ambalo lina dhamira njema, walikuwa wanawarushia mawe viongozi wa machinga ili kutaka kuanzisha tafrani, hivyo ieleweke kuwa watu hao sio wamachinga halisi,” alisema Lusinde.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makalla, alisema utaratibu wa kuwapanga machinga katika mkoa huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa, akiwapongeza wafanyabiashara na viongozi wao katika baadhi ya maeneo kwa kukubali kuondoka na kushirikiana na serikali.
“Viongozi tumejifunza kwamba elimu ikitolewa, mkija na hoja haitohitaji nguvu na hiyo ndiyo siri ya mafanikio katika Mkoa wa Dar es Salaam.
"Wametuelewa, vibanda vingi vinavunjwa na wao wenyewe wanahama na kazi yetu sasa tumejipanga kuhakikisha kwamba kila eneo wanalohamia huduma za msingi kama umeme, maji, ulinzi na magari ya kushusha abiria katika maeneo hayo yanakuwapo ili biashara zifanyike.
“Leo (jana) mtu aliyekuja miaka mitano nyuma akaambiwa ile pale ndiyo IFM au CBE anaweza akahisi amepotea na kukuambia umempeleka sehemu nyingine, hata mji wenyewe ungekuwa ni binadamu tungesema umepumua kwa sasa.
"Ukiwa IFM una uwezo wa kuona Wizara ya Elimu lakini zamani kulikuwa vibanda, moshi kila sehemu kulikuwa na vurugu,” alisema Makalla.