Dhuluma, kutukanwa na kupigwa ni baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wanaokopesha bidhaa za nyumbani. Wengi wa wafanyabiashara hao ni vijana ambao wamekuwa wakipita mitaani kukopesha watu vyombo, nguo na bidhaa nyingine kulingana na makubaliano na wateja. Miongoni mwa wafanyabiashara hao ni Hamisi Razak, Lucas Joseph na Kessy Ali, ambao kwa nyakati tofauti wamezungumza na Mwananchi kuhusu wanayoyapitia katika biashara hiyo inayowapa kipato, lakini yenye changamoto hasa wakati wa kudai madeni. Ili kupata bidhaa za kukopesha wateja mitaani, wafanyabiashara hao huzinunua kwenye maduka na wakati mwingine hupewa kwa mali kauli, wakilazimika kuacha vitambulisho ili kudhaminiwa na watu wanaofahamika na wenye maduka yaliyopo Kariakoo. Mapenzi kufidia deni “Niliwahi kumkopesha mama mmoja huko Manzese, alichukua bidhaa zenye thamani ya Sh30,000. Makubaliano yalikuwa atalipa Sh1,500 kila siku na kianzio ilikuwa Sh3,000, mwisho wa siku alihama nyumba bila kumaliza deni,” anaeleza Razak, aliyejikita katika biashara ya vyombo vya udongo (kauri). Akiwa na uzoefu wa miaka minne katika biashara, Razak anasema kuna siku mdeni wake alimtaka kimapenzi ili kufidia deni. “Kuna siku nilikwenda kudai deni, nikashangaa. Nilikaribishwa ndani wakati halikuwa jambo la kawaida, nikaingia na kukuta mama amevua nguo, ilinilazimu niondoke na kurudi kesho yake. “Awali, nilikuwa nashangaa na kujiuliza kwa nini nafanyiwa vituko, niligundua hawataki kumaliza madeni hivyo wanatafuta mitego ya kutokulipa,” anaeleza. Razak anasema kamwe hatasahau siku alipopigwa na mume wa mdeni wake akimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe. “Hii ilitokea Tandale, nimemaliza kukopesha vyombo nikaanza kudai fedha, kwenye nyumba moja nilikuwa nadai Sh50,000. Nilimkuta mume wa mkopaji nikamuuliza kuhusu mkewe, hakuuliza kitu akaanza kunishambulia akidai natembea na mkewe na ndani hawana maelewano. “Kuna wateja wanakopa hawasemi kwa waume zao kama wanadaiwa, matokeo yake ukiingia vibaya unapigwa kama mwizi wakati umekwenda kufuata mlichokubaliana,” anasimulia Razak. Makubaliano ya malipo Katika ukopeshaji hakuna mkataba wa maandishi, hivyo hata pale mdaiwa anaposhindwa kulipa huwa vigumu kumchukulia hatua za kisheria. “Unapokwenda kumdai mtu asipokulipa huna cha kumfanya kwa sababu ya kutokuwepo maandishi wakati wa kukabidhiana,” anasema Joseph, anayekopesha redio. “Wakati wa kukopa wanakupa matumaini ya kulipa. Huwa tunakubaliana malipo ya Sh1,000 kila siku. Mwanzoni hulipa vizuri, lakini baadaye hubadilika na kuwa wakali.” Mashtaka kwa mjumbe Usumbufu unapozidi, wafanyabiashara hao huwashirikisha wajumbe wa mitaa ili kupata msaada. “Nilimpeleka kwa mjumbe wa mtaa dada mmoja baada ya kunisumbua kwa muda mrefu. Alichukua meza ya kioo ya Sh100,000, alilipa kianzio Sh35,000, baadaye akanilipa Sh5,000 akaanza kusumbua. Kila ninapokwenda huwa simkuti na wakati mwingine hujificha,” anasimulia Ali. “Majirani zake walinishauri niende kwa mjumbe, huko nilikuta ana kesi tatu za kudaiwa. Nikapewa barua niende Serikali ya Mtaa, aliitwa akakataa kuwa hajawahi kukopa kwangu na anashangaa imekuwaje nimempeleka pale.” Imani za kishirikina Baadhi ya wateja hudai wafanyabiashara hao hutumia dawa katika biashara, jambo ambalo wao wanalipinga. “Nilikopa begi kwa Sh55,000, nilikuwa nikilipa Sh2,000 kila siku. Thamani ya begi lile Kariakoo ikizidi sana Sh35,000 nikapanga kumlipa Sh40,000. Hawa jamaa huwezi kuwadhulumu, hata ukisafiri mwaka ukirudi utamkuta anakusubiri. “Kuna jamaa yangu bingwa wa kutapeli lakini alifeli mipango yote. Alichukua feni, kila mtaa atakakopita anakutana na yule mfanyabiashara. Siku akiwa kazini hatokei, akiwa nyumbani hufika na daftari lake. Mwisho aliamua kulipa,” anasimulia Hussein Kasimu alipozungumza na Mwananchi akiwa Temeke. Akizungumzia tuhuma hizo mfanyabiashara Ali anasema; “Huwezi kopesha sehemu moja kila siku, naweza kopesha Vingunguti miezi mitatu nikahamia Ubungo, Kimara nikaenda Mbagala nikarudi Vingunguti tena. “Kuna mtu umemkopesha Buza akahamia Ubungo, nikihamishia kambi Ubungo tukakutana, hapo lazima unione mchawi.” Anasema baadhi ya wahudumu wa baa hukopa na kukimbia, hivyo ikitokea mfanyabiashara akapita maeneo ya baa hizo na wakakutana atasema ni ushirikina. Ugumu wa biashara Razak anasema huwa wanatembea umbali mrefu na hawakai maeneo ya jirani na wanakofanyia biashara. “Nakaa Mbagala, biashara nafanyia maeneo mengine, hili linasaidia kuepuka kujuana,” anasema. Kutokana na wakati mwingine kutokuwa na mtaji wa biashara anasema, “Ninapokusanya madeni sikopeshi hadi niwe na kiasi fulani. Kuna mwingine anamaliza deni akiwa amekusumbua miezi mitatu, anatafuta fedha anakulipa kwa pamoja. Huyu unaachana naye ili kuepuka usumbufu.” Changamoto nyingine anasema ni ya wakopaji kutokuwa wenyeji wa eneo husika, ambao wamekwenda kutembelea jamaa zao, hivyo kuwa vigumu kuwapata. Wasemavyo wakopaji Asha Salum, mkazi wa Vingunguti anasema mara nyingi muda wa malipo huwa jioni saa 10. Anasema ingawa malipo ni Sh1,000, bado wapo wanaoshindwa kulipa kutokana na kuwa na mikopo mingi au changamoto nyingine. Kwa upande wake, Mwanaidi Simbe, mkazi wa Temeke anasema kudaiwa ni kitu cha kawaida, akieleza baadhi ya bidhaa anazokopa ni kwa ajili ya kwenda kuwatunza marafiki kwenye sherehe. “Wapo waliokopeshwa televisheni na wakalipa kwa wakati, lakini wengine wanaishia kukopesha mashuka, mapazia na vyombo vya kupikia ambavyo havina gharama kubwa baada ya kuona wanadhulumiwa na kusumbuliwa,” anasema Zabibu Idd, mkazi wa Mabibo. Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti wa Serikali za Mtaa jijini Dar es Salaam, Juma Mwingamno ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuwa na tahadhari ili kuepuka usumbufu. “Wakimkuta mama wananadi bidhaa kwa kumwambia siyo lazima kutoa fedha yote taslimu. Wanakopeshana watu wasiojuana tabia,” anasema. Mwingamno anasema matukio ya kudhulumiana hutokea kwa sababu ya kutokufahamiana kiundani, kutokushirikisha wajumbe wa mtaa na mashahidi. Mchumi anena Mshauri wa Biashara na Maendeleo, Samwel Wangwe anasema kiuchumi wafanyabiashara hao wanajiangusha kwa sababu mkopeshaji anatoa unafuu kwa mnunuaji na kwake anajikuta anauza vitu vingi kwa faida ndogo. “Mkopeshaji anaweza kuona amefanya biashara kwa kuuza vitu vingi, lakini ikitokea asipolipwa kwa wakati inamuumiza kwa sababu baada ya muda mfupi mtaji unaweza ukakata na mkopaji akawa amechukua mali ya mtu bure,” anasema Wangwe. Anasema wakopeshaji wanatakiwa kuwa na watu wa kuwasimamia kisheria, hata ikitokea amedhulumiwa anaweza kusaidiwa. “Wanakutana na matukio ya kutapeliwa na kudhulumiwa kutokana na kutokuwa na utaratibu mzuri, wakiwa na taasisi inayowatetea ni rahisi hata kwenda kudai na ikiwezekana kuchukua kile kilichouzwa kikapigwa mnada na mdai akapewa kilicho chake,” anasema Wangwe.