Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Misri yafanya kweli Maonesho Sabasaba

927d92d9a5d63a7f90016a5d9f33871b.jpeg Misri yafanya kweli Maonesho Sabasaba

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kampuni 3,200 zimethibitisha kushiriki Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoanza leo kwenye Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa usafiri wa abiria wa mabasi ya mwendokasi kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi katika viwanja hivyo.

Alisema kampuni 1,800 kutoka nchi 22 na 1,400 za Tanzania zimethibitisha kushiriki maonesho hayo. Kwa ushiriki kutoka nje, alisema Misri inaongoza kwa kusajili kampuni 65, ikifuatiwa na China yenye kampuni 22 na Pakistan kampuni 12. Kwa mujibu wa Latifa, nchi nyingine zina kampuni hapa nchini lakini pia zimeleta kampuni zao na washiriki wao kutoka nje.

“Mwaka huu mwitikio ni mkubwa ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita, hii yote inatokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuutangaza utalii kimataifa kupitia filamu ya Royal Tour ambayo imewavutia wafanyabiashara kushiriki maonesho mwaka huu na ili wajionee hali halisi iliyopo nchini,” alisema.

Latifa aliwahakikishia washiriki usalama wa kutosha kwa kuwa Tantrade imejipanga kuhakikisha usalama wa washiriki na mali zao unazingatiwa. Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo akiwa ni kiongozi wa wilaya mwenyeji wa maonesho hayo aliwataka wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuchangamkia fursa zitokanazo na maonesho hayo.

“Leo (jana) tumezindua njia ya mabasi yaendayo haraka kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Sabasaba, kesho (leo) itazinduliwa ya Gerezani hadi Sabasaba, lengo letu ni kuwarahisishia wafanyabiashara wetu na wateja kuhudhuria Maonesho ya Sabasaba bila msongamano wa foleni barabarani, sasa na nyinyi tumieni fursa hii kununua na kuuza lakini msisahau Agosti 23, 2022 tuna jambo letu kwani jambo la mama ni jambo letu,” alisema Jokate.

Kiingilio katika maonesho hayo kwa wakubwa ni Sh 3,000 na watoto Sh 1,000.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live