Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Misitu yachangia pato la taifa bilioni 373/-

D8a48ef905b9a569017bf4fdc4cf0eed Misitu yachangia pato la taifa bilioni 373/-

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amesema sekta ya misitu na nyuki nchini imechangia takribani Sh bilioni 373 katika pato la taifa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018 mpaka 2020.

Katika ziara yake hivi karibuni mkoani hapa ambapo pia alizindua shambala la miti Silayo, wilayani Chato, Waziri Ndumbaro alisema sekta ya misitu imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na ndiyo maana serikali inaendelea kuunga mkono uwekezaji katika sekta hiyo.

Alisema hadi kufikia sasa sekta ya misitu na nyuki imekuwa ikichangia katika pato la taifa takribani Sh bilioni 5.2 kwa mwaka kama Kodi ya Ongezeko la Thamani(VAT) kutokana na biashara ya bidhaa za misitu.

“Sekta hii ni muhimu sana, maeneo ambayo yalipandwa miti siku nyingi yanafaidika sana na misitu, mfano Halmashauri ya Mafinga inapata mapato ya ndani ya Sh bilioni 1.3 kwa mwaka kutokana na misitu,”alisema na kuongeza kwamba: Shamba la miti la Silayo toka limeanzishwa limeweza kutoa ajira 800 kwa mwaka na inakadiriwa uvunaji utakapoanza litaweza kutoa takribani ajira 30,000 kwa mwaka na kaya zaidi ya 9,000 zinazozunguka eneo hilo zitafaidika moja kwa moja.

Kamishina Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania(TFS), Profesa Donston Silayo alisema uvunaji wa miti katika shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 69,756 unatarajiwa kuanza rasmi ndani ya kipindi cha miaka 14 ijayo.

Ikumbukwe kuwa, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 sekta ya misitu nchini iliingizia serikali Sh bilioni 130 sawa na asilimia 3.5 ya Pato la Taifa ikiwemo asilimia 5.5 ya fedha za kigeni na imeweza kutoa ajira kwa Watanzania takribani milioni moja mpaka sasa.

Aidha taarifa zinaonesha asilimia 55 ya eneo la nchi sawa na hekta milioni 48 zimefunikwa na misitu, huku asilimia 36 ya eneo hilo limetengwa kwa shughuli za uhifadhi inayojumuisha misitu ya uhifadhi 463, hifadhi za taifa 22, mapori ya akiba 23 na mapori tengefu 14.

Chanzo: habarileo.co.tz