Misitu ya hifadhi 11 imetambuliwa na Serikali ya Zanzibar na kutumika kikamilifu kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya utalii na hifadhi ya maliasili za viumbe mbalimbali.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Khamis Shaame wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Kikwajuni (CCM), Nassor Salim Jazira aliyetaka kufahamu misitu ya hifadhi inayotambuliwa na serikali na juhudi za kuilinda ikiwamo kupambana na uvamizi na ukataji miti.
Aliutaja Msitu wa Hifadhi wa Jozani wenye ukubwa wa hekta 6,688 ambao umetambuliwa na kuwa hifadhi ya taifa na kutembelewa na wageni mbalimbali wakiwemo watalii.
Alisema msitu huo umehifadhi utajiri mkubwa wa baianowai ikiwamo viumbe adimu pamoja na wanyama kama kima punju ambao wanalindwa kutokana na tishio la kutoweka.
''Msitu wa Jozani unatambuliwa rasmi kuwa ni hifadhi ya taifa na kwa nyakati tofauti umepata tuzo ya kimataifa katika uhifadhi wa viumbe ambavyo vipo katika hatari ya kutoweka pamoja na miti maarufu,'' alisema.
Aidha, aliutaja Msitu wa Hifadhi ya Kiwengwa Pongwe wenye ukubwa wa hekta 3,406, wizara imeanza kuchukua hatua mbalimbali za uhifadhi wake kutokana na tabia ya baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kuvamia na kukata miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.
''Msitu wa Hifadhi ya Kiwengwa sasa unatambuliwa rasmi kuwa upo katika hifadhi ya taifa, ambapo wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hiyo wamepewa elimu juu ya kudhibiti athari za mazingira,'' alisema.
Misitu mengine ya hifadhi ni Jambini Muyuni hekta 4,214, Ufufuma Pongwe hekta 1,988 na Masingini hekta 566.
Mwingine ni Msitu wa Hifadhi wa Ngezi uliopo Pemba wenye ukubwa wa hekta 2,900, Msitu wa Vumawimbi na Ras Kiuyu.
''Misitu hii imekuwa ikilindwa kwa kufanyika doria mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na matukio ya uhalifu kwa wananchi kuvamia na kukata miti kwa matumizi ya kuni na mkaa,'' alisema.
Khamis alisema mikakati ya wizara hiyo ni kuendelea kuimarisha hifadhi hizo ambazo huingiza mapato zaidi ya Sh bilioni moja na watalii 80,000 wanaotembelea vivutio hivyo.