Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miradi ya taka sifuri kutengeneza ajira 18,000

Da2fa8c1d3df1cfb64af1d6b81e38626 Miradi ya taka sifuri kutengeneza ajira 18,000

Wed, 17 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MIFUMO ya Taka sifuri imeonekana inaweza kutengeneza ajira zaidi ya 18,000 kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, utafiti umebainisha.

Utafiti huo mpya umefanywa na shirika lisilo la kiserikali la GAIA, ambapo pia umeonesha kuwa miji inayowekeza kwenye miradi ya taka sifuri na sera, inatengeneza ajira nyingi kijani, ikiwa na faida kubwa na kupunguza uharibifu na uchafuzi wa mazingira na kuboresha afya ya jamii.

Taka sifuri ni mfumo wa usimamizi wa taka ambao unatoa kipaumbele cha kupunguza taka na urejeshaji vifaa kazi kwa lengo la kujenga uchumi imara, kuondoa utupaji wa taka kufikia sifuri.

Mwandishi wa ripoti ya utafiti huo ambaye ni Mkurugenzi wa Sera na Sayansi kutoka GAIA, Dk Neil Tangri alisema, “Mfumo wa taka sifuri unatoa mkakati mzuri wa kutengeneza ajira bora na kupunguza uchafuzi na uharibifu wa mazingira. Ni ushindi mara tatu kwa uchumi, mazingira na jiji kwa ujumla.”

Alisema utafiti unasema kuwa kama jiji la Dar es Salaam lingerejesha asilimia 80 ya taka rejeshi ndani ya taka zizalishwazo, jiji lina uwezo wa kutengeneza ajira mpya zaidi ya 18,000.

“Utafiti unaweka wazi kuwa kilicho kizuri kwa mazingira pia ni kizuri kwa uchumi. Mikakati ya taka sifuri imepata maksi za juu zaidi kwenye faida za kimazingira na utengenezaji ajira nyingi kupitia eneo lolote la usimamizi wa taka,”alisema.

Akielezea faida za mfumo wa taka sifuri walizobaini kwenye utafiti ni kuwa utumiaji tena wa taka, unatengeneza zaidi ya mara 200 ya ajira kuliko madampo. Uchomaji na urejeleshaji hutengeneza karibu mara 70 ya ajira kuliko madampo na uchomaji.

“Utengenezaji upya wa taka hutengeneza mara 30 zaidi ya ajira kuliko madampo na uchomaji. Kwa upande mwingine, mifumo ya utupaji inategemea na uchomaji taka kwa nishati na madampo ili kukabiliana na vyanzo vingi vya taka na kusababisha gharama kubwa za kiuchumi na matokeo ya kimazingira,”alisema.

Alsiema mifumo ya taka sifuri, sio tu inatengeneza ajira nyingi, inatengeneza ajira zilizo bora.

Tafiti zinaonyesha kuwa ajira katika mifumo ya taka sifuri huenda zaidi ya kazi za mikono, hutoa mishahara ya juu, hutoa nafasi zaidi za kudumu na kuboresha ubora wa maisha.

Kwa mfano, mfumo wa kibunifu wa taka sifuri ambao unatekelezwa na taasisi ya ndani isiyotengeneza faida, Nipe Fagio katika jamii zenye kipato cha chini jijini Dar es Salaam, unaendana na usimamizi wa mazingira na ujumuishaji wa jamii, kwa kufanya kazi na watu walio katika mazingira magumu na kuishirikisha jamii katika ufumbuzi mzuri na wa gharama nafuu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio, Ana Le Rocha alisema, “Mfumo wa Taka Sifuri jijini Dar es Salaam una uwezo wa kutengeneza ajira 40 katika kila jamii yenye kaya 5,000 kwa makadirio, kwa kuzalisha kipato ndani ya jamii na kuzidi kuleta matokeo chanya katika kuijengea jamii uwezo na elimu.”

Chanzo: habarileo.co.tz