Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miradi ya maji 58 kugharimu bil. 4.9/-

MAJI HUDUMAA Miradi ya maji 58 kugharimu bil. 4.9/-

Thu, 4 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) mkoani Dodoma, umelenga kutekeleza miradi ya maji 58 yenye thamani ya Sh. bilioni 4.986 kwa mwaka ujao wa fedha.

Akizungumza jijini hapa jana, Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Dodoma, Dk. Godfrey Mbabaye, alisema miradi hiyo wataitekeleza katika maeneo mbalimbali ya wilaya saba za mkoa huo.

Dk. Mbabaye alisema kuwa kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 2.59 ni kwa ajili ya miradi 28 ambayo ni endelevu, Sh. milioni 345 zimetengwa kwa ajili ya kukarabati miradi 10, Sh. milioni 513 za upanuzi wa miradi na Sh. bilioni 1.5 ni kwa ajili ya ujenzi wa miradi mpya.

“Tunatarajia kutumia zaidi ya Sh. bilioni 4.986 kwa ajili ya kutekeleza miradi 58 kwa mwaka wa fedha ujao, lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata maji yaliyo safi na salama ambayo yanakidhi viwango vinavyotakiwa,” alisema.

Dk. Mbabaye, akizungumzia utekelezaji wa miradi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka huu, alisema walikuwa wanatekeleza miradi 40 yenye thamani ya Sh. bilioni tisa ambayo hadi sasa mingi imeanza kutoa huduma.

Alisema kati ya miradi hiyo, ipo ambayo haijaanza kutoka maji kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuharibika kwa miundombinu ya barabara ambayo ilisababishwa na mvua kubwa kunyesha, hivyo kushindwa kufika maeneo ya miradi kwa wakati.

Alisema upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dodoma ni wa asilimia 62, lakini wanatarajia kufikia Juni 30 mwaka huu, kiwango kitafika asilimia 70.

“Tunatambua kuwa wananchi wanatumia maji yenye magadi katika baadhi ya maeneo, ili kumaliza tatizo hilo, tutavuta maji kutoka Kijiji cha Msisi ili tuyachanganye na yale wanayoyatumia kwa sasa, hii itakuwa suluhisho la tatizo hili kwa wakazi wa Hombolo,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live