Moja ya hatari inayowakumba watu wanaoishi jirani na hifadhi ni kifo, uharibifu wa mazao na mazao pamoja na mifugo kuuawa.
Kwa mfano, takwimu za idara ya wanyamapori zinazoanzia mwaka 2012 hadi 2019, zinataja watu waliouawa na wanyama hao ni 1,069.
Aidha, 642 wakajeruhiwa huku ekari 41,404 za mazao mbalimbali zikiharibiwa, mifugo 792 kuuawa na wanyamapori na Shilingi bilioni 4.6 zililipa fidia kwa waathirika.
Uharibifu huo unatokana na wanyama kupita kutoka eneo moja kwenda jingine kutafuta mahitaji, jambo ambalo wadau wanalitafutia ufumbuzi, ikiwamo Taasisi ya Kusimamia Uhifadhi wa Tembo wa Kusini (STEP).
Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo kupitia mradi Tuhifadhi Maliasili, wameongoza au kufufua, shoroba ya tembo ya Kilombero inayopewa jina la Nyerere-Selous –Udzungwa.
Kwa zaidi ya miaka 10 ambayo wamefanya kazi kwenye eneo hilo wametumia mbinu mbalimbali kusaidia jamii, ikiwamo kuwa na miradi ya kufukuza tembo ili waendelee na kilimo.
Lakini, STEP imejenga shoroba ya kwanza ya kisasa ambayo itawekewa waya wa umeme na kulazimisha wanyama kupita kwenye njia maalum hifadhi ya taifa Udzungwa kwenda Hifadhi ya Taifa Nyerere hadi Pori la Akiba Selous.
Tayari wananchi wameshalipwa fidia kupisha ujenzi huo katika vijiji vya Kanyenja, Sole na Mang’ula A ambao wana miradi tofauti, pamoja na vikundi vya VIKOBA lengo ni kuwawezesha kiuchumi na kuwa na mbinu za kufukuza tembo.
Mratibu wa mradi wa kuboresha mahusiano kati ya tembo na watu wa STEP, Kim Lim anasema lengo ni kupunguza uharibifu wa mazao unaosababishwa na wanyama na kuwezesha wananchi kujiongezea kipato na kutoa elimu kwa wanafunzi.
“Tunafanyakazi na vikundi saba kwa miradi ya uzio wa mizinga ya nyuki, taa za umeme wa jua na uzio wa mabati kuzuia tembo wasiingie mashambani na vikundi 12 vya VIKOBA kuwezesha wananchi kuona faida ya uhifadhi,” anasema.
Kuhusu mizinga Lim anasema wana kikundi wamepewa elimu na kuwezeshwa na sasa wanauza asali na kupata fedha ambazo hugawana kwa kadri ya makubaliano.
“Kwenye VIKOBA tunafanyakazi na vikundi 12 vyenye wanachama 250 ambao asilimia 50 ni wanawake na vijana, tangu mwaka 2020 hadi sasa vinawasaidia kutatua changamoto zao,” anasema.
“Kabla ya VIKOBA hivi kama mwanachama akihitaji mkopo alikuwa anakopa Shilingi 50,000 kwa dhamana ya gunia la mpunga, anayemkopesha anabaki nalo kusubiri bei ipande ambalo analiuza 200,000 hadi 250,000 anapata faida zaidi ya Shilingi 100,000.
Kupitia VIKOBA watu hawachukua mikopo kwa udhamini wa mpunga, wanakopa na kurejesha baada ya miezi mitatu,” anafafanua Lim.
Aidha, ndani ya VIKOBA kuna fungu la jamii ambalo mtu akipata dharura kama kufiwa au kuuguliwa anaweza kuchukua mkopo wa dharura.
Kwa mujibu wa Lim, mikopo iliyotolewa kwa VICOBA ni zaidi ya Shilingi 7, 000,000 na wanakikundi walinunua hisa zenye thamani ya Sh. milioni 35, na kwamba kila wakinunua wanatumia kuchukua mikopo kwa ajili ya shughuli za kilimo na kurejesha.
“Kwa Kijiji cha Sole kuna mama ameanzisha mradi wa kuku na sasa wamefika 70, mwingine amejenga choo cha kisasa. Haya ni baadhi ya mafanikio makubwa. Pia wanapata elimu ya uhifadhi kwa shule za sekondari na msingi, tunawapeleka kwenda kutalii na kujifunza hifadhi za Udzungwa na Mikumi kutokana na namna wanavyofanya vizuri kweye mitihani hao, wanajifunza tabia za tembo na wakienda hifadhini wanaona,” anasema.
Aidha, anasema kwenye mizinga changamoto ni kukosa nyuki kutokana na mazingira yaliyopo ambayo nyuki hajitengenezea chakula chao wenyewe na kusababisha mizinga kukosa asali.
Kwa mujibu wa Lim, miaka mitatu ijayo wataanzisha vikundi 16 katika vijiji nane ili kuendelea kuwasaidia wananchi na wanashirikisha kwa kila kitu ili viwe endelevu hata mradi utakapokwisha.
Mtaalamu wa nyuki wa kikundi cha Njokomoni, Ahemed Churi, anasema tembo walikuwa kero na kukwamisha kilima ndipo lakini ufumbuzi umepatikana baada ya STEP kuwaelimisha.
Wamefundisha kutengeneza uzio wa pilipili kwa kuweka vitambaa ambavyo akinusa anapiga chafya na kurudi alikotoka, lakini baadaye waligundua na kuanza kugeuka kinyumenyume kuingia mashambani.
“Tukabuni mradi wa nyuki ukiweka mizinga tembo hawataingia, kwa ufadhili wa hifadhi ya Udzungwa tulipata mizinga 20 na baadaye STEP wakatupatia 100 ambayo tumeiweka umbali wa mita moja, iliyounganishwa na nyaya ambayo tembo akija akitikisa nyuki wanatoka na kuwang’ata kisha wanakimbia,” anasema.
Aidha, anasema mradi huo kwenye eneo la kilomita moja na mizinga 76 na yenye nyuki ni 19 pekee umekuwa na manufaa kwa kuwa zamani tembo walikuwa wanaingia kwenye mashamba lakini sasa wamewazuia.
Anasema mapato yao ni zaidi ya Sh. 300,000, akiomba wasaidiwe ili mradi uwe mkubwa ikiwamo kutambuliwa na Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS), ili wafikishe bidhaa kwenye masoko ya nje na ndani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’ula A, Junior Mponela, anasema uelewa wa wananchi umeongezeka na kwamba kwa sasa wananufaika na miradi mbalimbali na wanyama sio tatizo kubwa kama ilivyokuwa awali ndio maana wanalima maeneo ambayo kwa miaka mingi hawakuyagusa.
Michael Mkaranga ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Sole, anasema awali tembo walikuwa wanaharibu mazao yao mara kwa mara lakini kwa sasa kuna nafuu kubwa na jamii inaona faida kwa kuwa kutokana na vikundi vinavyowapa mikopo na mbinu za kufukuza tembo ambazo zinawaletea faida kama kufuga nyuki.
Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Kanyenja, Mohamed Mohamed, anasema asilimia 75 ya mradi wa kufufua shoroba uko kijijini humo na kwamba serikali imefanya jambo kwa kuwa tembo walikuwa wanaharibu mazao kikubwa na sasa wanalima maeneo ambayo kwa miaka mingi hayakuguswa.