Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miradi ya kimkakati kuifungua Tanga kiuchumi

Tangaaaaa Uchumi (600 X 299) Miradi ya kimkakati kuifungua Tanga kiuchumi

Wed, 6 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa barabara Tanga itakayounganisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Miradi hiyo inategemewa kupunguza gharama, muda wa safari na kurahisisha ufanyaji biashara ikiwamo kufikika kwa urahisi kwenye vivutio vya utalii. Pia, barabara hiyo kwa kuwa ni kiungo kizuri kati ya bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa, itachochea uchumi wa buluu.

Akuzungumza leo Machi 5, 2024 Meneja wa Tanroads Mkoa wa Tanga, Dastan Singano amesema miradi hiyo ni ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya Bagamoyo inayounganisha Mkange, Pangani na Tanga yenye urefu wa kilomita 256.

Amesema ujenzi huo ni sehemu ya Barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayounganisha Kenya na Tanzania kwa ukanda wa Pwani.

Ujenzi wa Barabara ya Handeni, Kiberashi, Kijungu, Chemba, Kwamtoro hadi Singida yenye urefu wa kilomita 434.33 inayojengwa kwa kiwango cha lami, unatekelezwa kwa awamu huku ya kwanza ikianzia Handeni hadi Mafuleta kilomita 20.

Awamu ya pili inaanzia Mafuleta hadi Kileguru kilomita 30 na awamu ya tatu ni kutoka Kileguru, Kiberashi, Kijungu, Chemba, Kwamtoro hadi Singida kilomita 384.33 itakayojengwa kwa mfumo wa EPC+F.

"Barabara ya Tanga hadi Pangani ujenzi ulikuwa unasuasua lakini baada ya Serikali kutoa fedha Januari 2024 zimemfanya mkandarasi kupata nguvu ya kutekelezaji mradi ule kwa kasi,’’ amesema Singano.

Amesema pia Serikali ina mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Mkata hadi kwa Msisi kilomita 36, barabara ya kutoka Old Korogwe kwenda Bombomtoni mpaka Mabokweni kilomita 127.

Na Barabara ya Soni, Bumbuli, Dindira hadi Korogwe kilomita 30 na ya Handeni kwenda Mziha ambayo tayari Serikali imeshatoa kibali cha kuanza ujenzi wa kilomita 20.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live