Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miradi ya Maendeleo sasa kufanyika bila mikwamo

FYDP Wajumbe wa timu ya kutafuta vyanzo vya mapato

Fri, 25 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imezindua Timu ya Kitaifa itakayozisaidia Wizara, Idara na Taassisi zake kupata fedha za kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati kwa kutumia njia mbadala kutoka sekta binafsi (National Facilitation Team).

Akizungumza wakati wa hafla hiyo jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Lawrence Mafuru mpango mpya uliobuniwa na Serikali wa kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi, umelenga kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo badala ya kutumia bajeti ya Serikali.

''Serikali imekuwa ikitekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ili kukuza uchumi na kuondoa umasikini kwa kutumia Bajeti ya Serikali lakini utaratibu huu umekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti ya Serikali na hivyo miradi mingi kupata fedha kidogo na kutokamilika kwa wakati’’. Alisema Mafuru.

Mafuru aliongeza kuwa, utaratibu huu utaiwezesha Serikali kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati na yenye uwezo wa kuzalisha mapato pasipo kutumia vyanzo vyake vya mapato moja kwa moja na kuiwezesha kuwa na uwezo zaidi wa kugharamia miradi ya kijamii ambayo haina sura ya kibiashara hususan ile inayoigusa jamii.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa (TAMISEMI), Dkt. Sixbert Mkama alisema timu hiyo italeta mageuzi makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini ambapo TAMISEMI imekuwa mtekelezaji na msimamizi mkubwa wa miradi mbalimbali nchini.

“Ninaiomba Timu hii iwajengee uwezo watendaji hususani Wakurugenzi wa Halmashauri katika maeneo ya uandishi wa maandiko ya miradi wanayokusudia kuitekeleza” alisema Bw. Mkama

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) Peter Malika alisema kipaumbele kikubwa cha Mfuko huo ni kushughulikia masuala mbalimbali ya uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango.

Malika aliongeza kuwa kwa kuzingatia mahusiano mazuri na Serikali, Mfuko huo umetoa shilingi milioni 460.4 ili kuwezesha Timu iliyozinduliwa kutekeleza majukumu kikamilifu ikiwemo kutoa msaada wa kiufundi kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kubuni miradi yenye sifa ya kuvutia uwekezaji kutoka kwa wadau nje ya Serikali.

Awali akiongea kabla ya uzinduzi wa Timu hiyo, Kamishina wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamaja alisema kuwa Wizara hiyo iliona ni vyema kuunda timu itakayofanya kazi ya kuainisha na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato yatakayo saidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alifafanua kuwa kiasi cha shilingi trilioni 40.6 kinatakiwa kupatikana kutoka katika Sekta Binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III) hivyo utaratibu huo mpya uliobuniwa na Serikali utaiwezesha Sekta Binafsi kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wan chi pamoja na kuiendeleza Sekta hiyo.

Dkt. Mwamwaja alisema kuwa Serikali kwa kutumia vyanzo vya sasa vya mapato (Traditional source) haiwezi kufanya mambo yote ya maendeleo, hivyo kupitia Alternative Project Financing (APF) itasaidia kutafuta vyanzo vingine vya mapato kupitia njia mbalimbali ikiwemo Hati Fungani zinazotolewa na Serikali Kuu pamoja na zile zinazotolewa na Taasisi za Umma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live